Thursday, August 19, 2010

Fedha Kwako Kitu Tasa

1.
Husaidiki mwanamke, fedha kwako kitu tasa,
Hupita mkondo wake, kwako kukaa hususa,
Mbegu mara zichimbuke, kuota kwako si ruksa,
Fedha kwako kitu tasa, mwanamke husaidiki.
2.
Haueleweki mwanamke, chako kisa na mkasa,
Vigumu ubadilike, ukaziona fursa,
Hayumkini ujengeke, bure mtu wajitesa,
Fedha kwako kitu tasa, mwanamke husaidiki.
3.
Labda igundulike, wewe kwa mtu asusa,
Wanaume wahongeke, jinsia iwe ngasa,
Mtu wa shika nishike, kazi kudata kipusa,
Fedha kwako kitu tasa, mwanamke husaidiki.
4
Ni ndugu wavumbulike, nao wanaokupapasa,
Au mwenzetu msagike,wazidi zimwaga posa,
Washikaji wakushike, ashikizo kuzigusa,
Fedha kwako kitu tasa, mwanamke husaidiki.
5.
Au mwenzetu mtakatike, wasaidia matasa,
Na wenye dhike mkeke, wewe huwapa mapesa,
Basi urehemeke, firdausi kugusa,
Fedha kwako kitu tasa, mwanamke husaidiki.
6.
Ungekuwa dume jike, mkwasi ungekuwa sasa,
Nyumba mwenyewe ushike,bila jicho kupepesa,
Na nduguzo wasaidike,sio kuwa kibubusa,
Fedha kwako kitu tasa, mwanamke husaidiki.
7.
Lisingelikuwa lake, gari usingelikosa,
Mtu bora maanake, kweli ungelitakasa,
Dubai nako ufike, kimataifa kuasa,
Fedha kwako kitu tasa, mwanamke husaidiki.
8.
Husaidiki mwanamke, naona bure najitesa,
Nitafute mbadalake, labda atanidodosa,
Na mimi nifurahike, mwenzi mwenye hamasa,
Fedha kwako kitu tasa, mwanamke husaidiki.

No comments: