Thursday, August 19, 2010

Pendo la binti tajiri

1.
Mimi nimelighairi, pendo la binti tajiri,
Ijapo pia mzuri, naichelea safari,
Kati isiwe ya shari, kwa joto na pia hari,
Pendo la binti tajiri, mtihani niloshindwa!
2.
Ni Lailatkadri, sikatai fakiri,
Uzuri wake dhahiri, na mwanya ulojiri,
Macho yake ya sifuri, hupenda kuyavinjari,
Pendo la binti tajiri, mtihani niloshindwa!
3.
Naona kama kamari, kucheza kitu hatari,
Utaisha ujibari, rijali niwe kadiri,
Nisijue adhuhuri, wala hiyo alasiri,
Pendo la binti tajiri, mtihani niloshindwa!
4.
Nitakuwa ni kafiri, mwajiriwa si mwajiri,
Sintoiona bahari, kwa macho yenye habari,
Nitawaza nisifikiri, kutend bila hiari,
Pendo la binti tajiri, mtihani niloshindwa!
5.
Usanii nivinjari, nikikosa kachumbari,
Kwa nje nitashamiri, ndani niwe kama ngiri,
Kitaniisha kiburi, nisiwe tena hodari,
Pendo la binti tajiri, mtihani niloshindwa!
6.
Kuizungusha sifuri, mistari kukithiri,
Na mizani na urari, wastani usijiri,
Nitaiona fahari, lakini si shwari na heri,
Pendo la binti tajiri, mtihani niloshindwa!
7.
Pendo la binti tajiri, mpenzi atahadhari,
Huingia taksiri, pasiwe na tena siri,
Na itazidi jeuri, uhofie yake shari,
Pendo la binti tajiri, mtihani niloshindwa!
8.
Nimeshindwa si mahari, ila yatakayodhihiri,
Heri nibaki kafiri, hilo nilishalikiri,
Niondokane na zari, cheo na umashuhuri,
Pendo la binti tajiri, mtihani niloshindwa!
9.
Nitamuoa fakiri, si mwana wa jemadari,
Asiye mwenye kiburi, pendo kwangu akikiri,
Tutatiana kabari, la mwili pia suduri,
Pendo la binti tajiri, mtihani niloshindwa!
10.
Maisha yawe ya kadri, na mwendo wa tahadhari,
Tutaivuka bahari, japo papa wadhihiri,
Tutakula tafakuri, kidogo kiwe cha heri,
Pendo la binti tajiri, mtihani niloshindwa!
11.
Tutapeana shauri, wangapi wana wajiri,
Tuwatunze kwa saburi, elimu waiabiri,
Uzeeni takbiri, waweza tupa kachori,
Pendo la binti tajiri, mtihani niloshindwa!
12.
Nawaasa mshairi, mwogope binti tajiri,
Labda awe dhahiri, awajali mafakiri,
Tena aso na kiburi, na mwoga kudhihiri,
Pendo la binti tajiri, mtihani niloshindwa!

No comments: