Thursday, August 19, 2010

Kiumbe kweli kijembe

1.
Kiumbe kweli kijembe, na wengine kama wembe,
Hawana lililo na chembe, ya tosheko wasigombe,
Hata vipi umpambe, lazima tope arambe,
Kiumbe kweli kijembe, japo kakosa mapembe!
2.
Mpambe mwana kijembe, na jambo nambe msambe,
Ni jipu lenye uvimbe, maumivu usiombe,
Kikwepe hicho kikombe, ni shubiri usiilambe,
Kiumbe kweli kijembe, japo kakosa mapembe!
3.
Ni mende mwenye uzembe, hata kwa vipi atambe,
Mwache kote ajigambe, mchana shida aimbe,
Mngoje Kigurunyembe,upuuzi wake ujumbe,
Kiumbe kweli kijembe, japo kakosa mapembe!
4.
Kiumbe sio mzembe, ila mwingi wa vijembe,
Msanii umuimbe, si mtamba sio tembe,
Usimuone ni ng'ombe, ana lake aliombe,
Kiumbe kweli kijembe, japo kakosa mapembe!
5.
Ni vigumu asigombe, akidai hata chembe,
Lake hutaka litambe, la kwako huona mwembe,
Kwa maslahi mpambe, ila kuzalisha mbembe,
Kiumbe kweli kijembe, japo kakosa mapembe!
6.
Na mikwara aichimbe, na fadhila azikombe,
Msambe nisambe kumbe, \snukrani usilambe,
Mja kachukue jembe, waachie ndugu wagombe,
Kiumbe kweli kijembe, japo kakosa mapembe!

No comments: