Thursday, August 19, 2010

Raha iko ndani yangu

1.
Sishughulishwi na ya nje, raha iko ndani yangu,
Ni vioja vilioje, kuwatazama wenzangu,
Hujiluliza wafanyaje, wawe kama watu-mungu,
Raha iko ndani yangu, sishughulishwi na ya nje.

2.
Wajua Kilwa Kivinje, hii si fatwa yangu,
Kila kitu mkivunje, nachieni nafsi yangu,
Makamu haya si njenje, kutibwirika si yangu,
Raha iko ndani yangu, sishughulishwi na ya nje.

3.
Raha iliyo kwa nje, kwangu mawingu na mbingu,
Siipati hata punje, na haipoozi moyo wangu,
Ila ndani niikunje, huona uzima wangu,
Raha iko ndani yangu, sishughulishwi na ya nje.
4.
Napenda walio nje, ila sio raha yangu,
Hili sio kitu uonje, ila tanafusi kwaangu,
Ni fikra zilo fiche, ndani mawazo yangu,
Raha iko ndani yangu, sishughulishwi na ya nje.
5.
Sishughulishwi na ya nje, furaha i ndani yangu,
Maisha msinipunje, Tao ni mwalimu wangu,
Na njia msiikunje, zipite hatua zangu,
Raha iko ndani yangu, sishughulishwi na ya nje.
6.
Hayaniwasi ya nje, si ya Mchina si Mzungu,
Weshaniita Machenje, naujua utu wangu,
Hata viungo mvunje, kuruka ni haki yangu,
Raha iko ndani yangu, sishughulishwi na ya nje.
7.
Nakera walio nje, hawaingii ndani yangu,
Huku na huko wahanje, hawaoni langu fungu,
Waache hao wabanje, mafua sio machungu,
Raha iko ndani yangu, sishughulishwi na ya nje.
8.
Nawaachia nyie ya nje, ya ndani ni haki yangu,
Siidai hata punje, kuleni yote mafungu,
Ila ya ndani msionje, ya kwenye wangu uvungu,
Raha iko ndani yangu, sishughulishwi na ya nje.

No comments: