Thursday, August 19, 2010

Taifa la wachuuzi

1.
Kunayo moja tu kazi, nayo si uzalishaji,
Ni tarafu ya uchuuzi, kila kijiji na kila mji,
Hatima yake ajizi, naona bora nihoji,
Taifa la wachuuzi, laweza kuendelea?
2.
Taifa la wachuuzi, bila ya wazalishaji,
Hata kwa chipsi viazi, Iwe nje uagizaji,
Naamini haliwezi, kuyakidhi mahitaji,
Taifa la wachuuzi, laweza kuendelea?
3.
Uchuuzi hauongezi, wala kupanua mtaji,
Kaziye ni matembezi, maikro kuifariji,
Kama wataka makuzi, lazima uzalishaji,
Taifa la wachuuzi, laweza kuendelea?
4.
Nchi yataka majazi, daraja walizo magwiji,
Bila kuifanya kazi, bidhaa kuzitaraji,
Kwenda mbele hatuwezi, tutabaki wafujaji,
Taifa la wachuuzi, laweza kuendelea?
5.
Taifa la wanunuzi, tena bila wauzaji,
NI taifa angamizi, liso usasahishaji,
Duni wake viongozi, hawafai kutaraji,
Taifa la wachuuzi, laweza kuendelea?
6.
Sio nchi ilo azizi, ya wageni kuja hiji,
Si pahala pa uzuzi, jipya kamwe haliji,
Ni mahala pa wakwezi, wakulima na walaji,
Taifa la wachuuzi, laweza kuendelea?
7.
Nchi yataka darizi, malengo na upangaji,
Watu wataka malezi, na kuengwa makuaji,
Ardhi yataka wekezi, udumu uzalishaji,
Taifa la wachuuzi, laweza kuendelea?

8.
Sasa yetu kubwa kazi, tuubebe uzalishaji,
Tufanye maamuzi, kwenye miji na vijiji,
Kisha tuanze kazi, Kukidhi yetu mahitaji,
Taifa la wachuuzi, laweza kuendelea?

No comments: