Thursday, August 19, 2010

Kaokoa mstarini

1.
Amechupia mtani, hatari kuiondoa,
Ilikuwa kimiani, ndani limeshaingia,
Kapiga abautani, mstarini kaokoa,
Kaokoa mstarini, nusura lingeingia!
2.
Beki huyu namba wani, goli hajaliachia,
Ajua wajibu nini, mwepesi kujitolea,
Uvivu ni abadani, kwake haujaingia,
Kaokoa mstarini, nusura lingeingia!
3.
Macho yake amini, kurunzi ilotimia,
Huona yote yakini, kiwanjani kitokea,
Ni mwepesi na makini, hawezi kukuachia,
Kaokoa mstarini, nusura lingeingia!
4.
Ukimkuta njiani, huwezi ukamjua,
Utadhani afkani, majinusi asojua,
Ila pale kiwanjani, ni nani wa kumvaa?
Kaokoa mstarini, nusura lingeingia!
5.
Ni kama mashinegani, risasi anavyofyatua,
Hurudi nyuma amini, washambulizi kadhaa,
Hawathubutu kughani,shambulizi huachia,
Kaokoa mstarini, nusura lingeingia!
6.
Tumekula na yamini, kipa tutamsaidia,
Vijana wote makini, wajua pa kuanzia,
Hawapiti mstarini, chenga zitawachengua,
Kaokoa mstarini, nusura lingeingia!
7.
Mechi hii ni kuwini, kushindwa tumekataa,
Tutahaha uwanjani,hadi golini kwingia,
Nyuma ni mwiko jamani,mbele nd'o pa kuingia,
Kaokoa mstarini, nusura lingeingia!
8.
Kikosi chetu auni, aali kimetimia,
Tunataka na nishani, nchi kuitumikia,
Ni kama tupo vitani, adui hatokimbia,
Kaokoa mstarini, nusura lingeingia!
9.
Kitali hiki yakini, kama tunakirudia,
Walojifanya wahuni, mbona tulishawatoa,
Na wasiojiamini, majuzi tuliwakataa,
Kaokoa mstarini, nusura lingeingia!
10.
Anatamba kapteni, machachari alokuwa,
Azidi kujiamini,dakika zikijongea,
Tunamtia imani,kombe tunalichukua,
Kaokoa mstarini, nusura lingeingia!
11.
Makosa tumebaini, kocha anachuchua,
Na mwilini na moyoni, mbalanga zimepungua,
Anajaza akilini, ushindi kuuchukua,
Kaokoa mstarini, nusura lingeingia!
12.
Mshairi wa kanuni, mwamini akikwambia,
Hapo ulipo chooni, shilingi waichezea,
Tokea huku uwani, mamboutajionea,
Kaokoa mstarini, nusura lingeingia!

No comments: