Thursday, August 19, 2010

Kumwoa Mzungu si Kazi

1.
Isiwe kizunguzungu, kumwoa Mzungu si kazi,
Ninawaambia wanangu,kuoa sio mapenzi,
Ila cha fedha chungu,ndio wake ufumbuzi,
Kumwoa Mzungu si kazi, kibarua kumtunza!
2.
Mzungu ataka fungu, ila sio fumanizi,
Huzipenda nyanya chungu,ila hapendi mchuzi,
Ushungi kwake ni pingu, hupenda kichwa cha wazi,
Kumwoa Mzungu si kazi, kibarua kumtunza!
3.
Hazipapatikii dengu, wala si mlaji wa nazi,
Feri kachukue changu, vibua kwake maudhi,
Hajui pikia chungu, mkaa kwake majonzi,
Kumwoa Mzungu si kazi, kibarua kumtunza!
4.
Mzungu hapendi majungu, kwa hilo nampa pengezi,
Wala hazijui kungu, kukurembulia kwa wizi,
Usimletee mkungu, kumenya ndizi hawezi,
Kumwoa Mzungu si kazi, kibarua kumtunza!
5.
Humwelewa nungunungu, ila mishale hauzi,
Huziogopa na pingu, basi usijekuwa mwizi,
Na mapanga na marungu, si Mkurya hayawezi,
Kumwoa Mzungu si kazi, kibarua kumtunza!
6.
M\zungu chake si changu, hili analimaizi,
Usifiche kwenye mvungu, atakuona jambazi,
Benki peleka mafungu, na usifanye uchuuzi,
Kumwoa Mzungu si kazi, kibarua kumtunza!
7.
Ni mtu wa wanguwangu, halitaki bumbuwazi,
Na humlipuka wengu, ukimletea uchizi,
Ama zako ama zangu, huo ndio uamuzi,
Kumwoa Mzungu si kazi, kibarua kumtunza!
8.
Wengine husema mchungu, haruhusu matumizi,
Tena hapendi ukungu, adai sana uwazi,
Ukifunika kwa mkungu, budi afanye uchunguzi,
Kumwoa Mzungu si kazi, kibarua kumtunza!
9.
Nawajuza watu Ndungu, pia na wa Mkomazi,
Mvielewe vifungu, msijeshindwa kazi,
Sio wenzetu wazungu, kuishi nao ni kazi,
Kumwoa Mzungu si kazi, kibarua kumtunza!

No comments: