Thursday, August 19, 2010

Kismati mara moja,

1.
Ukibahatika tena, kaushukuru mkaja,
La leo sio la jana, na wala hili si kioja,
Na kuja ni kujaana, kupishana si useja,
Kismati mara moja, mwaka ujao kiroja!
2.
Kipofu mwezi kuona, kachelewa jenga hoja,
Na sasa giza aona, Han teja wala tija,
Huona asichoona, na kusifu lisokuja,
Kismati mara moja, mwaka ujao kiroja!
3.
Mtu kama akili hana, hudharau lenye tija,
Akasifu liso maana, hata hekima kufuja,
Pepoze sio mwanana, Ni mtu wa kwenda na kuja,
Kismati mara moja, mwaka ujao kiroja!
4.
Hajengi lenye maana, wala hatimizi haja,
Huona walo mabwana, na kujifanya yeye mteja,
Haukatai utwana,ili awe na mirija,
Kismati mara moja,mwaka ujao kiroja!
5.
Kismati hutoona, kikikujia mara moja,
Yako hayawezi fana, bahati haitokungoja,
Mtazidi kupishana, na wa juu chini kuja,
Kismati mara moja, mwaka ujao kiroja!
6.
Mambo mchana kusana, hata za juja na majuja,
Ustawi mwana sana, uvivu hauna tija,
Neema kama hazina, kutunzwa jambo la haja,
Kismati mara moja, mwaka ujao kiroja!
7.
Kismati sintokana, hili kiungo daraja,
Ni kukosa na kufana, kuvua na kuvaa koja,
Kiumbe aso mtwana, hajifunzi kwa lahaja,
Kismati mara moja, mwaka ujao kiroja!
8.
Kismati muamana, huja hakiwindwi mja,
Ila yataka amana, pale kwako kitapokuja,
kushika ukikiona, tena sio kwa rejareja
Kismati mara moja, mwaka ujao kiroja!

No comments: