Thursday, August 19, 2010

Hautonielewa

1.
Si mtu wa kudhania, wala si wa kuvamia,
Ni mpole wa tabia, na mvivu wa hatua,
Sina ninalokimbia, wala ninalokimbilia,
Hautonielewa, tafuta 'ticha' mwingine!

2.
Elimu yangu dunia, digrii yangu tabia,
Fikra zangu ni dua, ushauri msamaha,
Si mtu wa kulilia, wala wa kufukuzia,
Hautonielewa, tafuta 'ticha' mwingine!
3.
Darasani nikingia, wajinga huwaondoa,
Wakabaki wanojua, toka walipozaliwa,
Neno nikilitoa, wao hulipigania,
Hautonielewa, tafuta 'ticha' mwingine!
4.
Wazito kwenye kujua, macho yao hufumbua,
Na wale wasiosikia, mara kitu hung'amua,
Na waioona njia, tahamaki wanajua,
Hautonielewa, tafuta 'ticha' mwingine!
5.
Kanzu niliyoivaa, kisomo imeptia,
Yajua msiyoyajua, mwilini imetulia,
Kamwe haitawaringia, wala kuwafunulia,
Hautonielewa, tafuta 'ticha' mwingine!
6.
Masomo yangu murua, watu huchekelea,
Wengi huja kudhania, kuna kitu wameambua,
Kumbe kwao hupitia, na mbele yakaendelea,
Hautonielewa, tafuta 'ticha' mwingine!
7.
Najua hawataelewa, hadi wanapojifia,
Kizazi kinachofatia, ndicho kitakachogundua,
Na mimi mpita njia, wajibu wangu najua,
Hautonielewa, tafuta 'ticha' mwingine!
8.
Maswali yangu ulua, ni migodi ilojaa,
Vito vilivyochaguliwa, bora mtu kuvitwaa,
Wanaoyachanganua, thamani njema hupewa,
Hautonielewa, tafuta 'ticha' mwingine!
9.
Mtihani wanaopewa, ni maisha kujua,
Na watu kuwaelewa, jinsi ya kuwachukulia,
Na kisha Afu kufaa, mmoya kumwabudia,
Hautonielewa, tafuta 'ticha' mwingine!
10.
Neno langu zingatia, utu utaufikia,
Hatua zangu fwatia, njia bora utajua,
Majibu yangu tumia, yote utakujajibiwa,
Hautonielewa, tafuta 'ticha' mwingine!
11.
Njia za mkato zafaa, kwa wale wasiojua,
Fupi refu linakuwa, na thawabu zake kujaa,
Muumba anatujua, hili halijambua,
Hautonielewa, tafuta 'ticha' mwingine!
12.
Beti zangu zatimia, mbele sintoendelea,
Daawa nimewapatia, yabaki kufwatilia,
Dua ninawaombea, mpate kuelekea,
Hautonielewa, tafuta 'ticha' mwingine!

No comments: