Thursday, August 19, 2010

Kisima chenu cha fikra

1.
Mnaopenda vya bure, anzeni kushangilia,
Haya hapa ya bwerere, ruksa kuvichukua,
Wanayaweza ngedere, kwenu halitowastua,
Kisima chenu cha fikra, choteni, kunyweni mtosheke!
2.
Sio Wachagga si Wapare, miteremko mwatumia,
Si Wamasai si Wakwere, vya bure waporomoshewa,
Yanini kiherehere, malipo kutarajia,
Kisima chenu cha fikra, choteni, kunyweni mtosheke!
3.
Zimejaa ni bwerere, msiache kukimbilia,
Pasina kiherehere, ndoo tieni na kutoa,
Mhifadhi na mchore, akilini kuzitia,
Kisima chenu cha fikra, choteni, kunyweni mtosheke!

4.
Ila vichwa msifure, hamjui msojua,
Bunduki sio gobore, mwaweza kujilipua,
Na Dar sio Harare, udikteta si tabia,
Kisima chenu cha fikra, choteni, kunyweni mtosheke!
5.
Ninamuenzi Nyerere, akili alitumia,
Afrika nani sare, na yeye kulingania?
Vipi fikra tugure, bila kuzifikiria,
Kisima chenu cha fikra, choteni, kunyweni mtosheke!

6.
Viazi sio vibere, ladha ukijagundua,
Uhuni sio ukware, fumanizi likiuumbua,
Cha kulipa si cha bure, hasara hutoijua,
Kisima chenu cha fikra, choteni, kunyweni mtosheke!

7.
Fikiri ndio kusare, lugha ukishaijua,
Naihofia Lahore, japo mie Mtanzania,
Mengine yote wapore, ila fikra mtaumia,
Kisima chenu cha fikra, choteni, kunyweni mtosheke!
8.
Kazi mbaya si kazi bure, usia ninautoa,
Maradhi kama ni ndere, mbwani chozi kukufichua?
Ushirikina si gere, ila kuuza ubaya,
Kisima chenu cha fikra, choteni, kunyweni mtosheke!

No comments: