Monday, August 20, 2012

Hadhi ya maji kujua




Ukitaka kuijua, isumbuayo kadhia,
Kijijini kuingia, kisha maji kullia,
Nawe ukajaimbiwa, wimbo wa kiu na njaa,
Hadhi ya maji kujua, ukose hata ya kunywa!

Halafu ikatokea, kanzu umeichafua,
Wataka doa kutoa, maji adimu yakawa,
Tayamamu kunuia, hali bado wazubaa,
Hadhi ya maji kujua, uchafu ukishajitia!

Kinamama wanalia, kilomita watembea,
Si moja ninakwambia, hizo zaweza kuwa kadhaa,
Alfajiri kujitoa, kudamka wakimbia,
Hadhi ya maji kujua, umbali ukitembea!

Hubakwa kwenye majia, na wengine kuuawa,
Na nyumbani kuibiwa, usalama kusinyaa,
Maisha kuwa balaa, na zikachanika ndoa,
Hadhi ya maji kujua, umbali ukitembea!

Nguo chafu utavaa, harufu zinazotoa,
Jasho lililogandia, tena gumu kulifua,
Kitambaa kufubaa, cheupe cheusi kuwa,
Hadhi ya maji kujua, ukose ya kufulia!

Kwenye miji wafulia, vyoo vibovu kujaa,
Vinyesi vinatembea, watalii vimekuwa,
Vyatisha kwenye njia, muumini waduwaa,
Hadhi ya maji kujua, ingia choo bila maji!

Misikiti hukimbiwa, maji adimu yakiwa,
Ibada haitakuwa, bila maji kujitia,
Usafi waamriwa, vingine haitakuwa,
Hadhi ya maji kujua, msikiti hukimbiwa!

Kodi wanajilipia, maji yazidi potea,
Na ahadi zatolewa, pembeni kwenda tokea,
Maonyesho kwenye njia, sinema bure twapewa,
Hadhi ya maji kujua, usiwe na ya kuogea!

Twakukabidhi Radhia, kuiondoa kadhia,
Mwelekeo wadumaa, suka njia kapotea,
Imebaki majaliwa, salam kujipatia,
Hadhi ya maji kujua, umbali ukitembea!





No comments: