Monday, August 20, 2012

Taifa pasipo baba


Taifa bila wazazi, mambo huenda mrama,
Kumebakia walezi, tena wasiojituma,
Na bahari ya machozi, wana wake wanalia,
Taifa pasipo baba, yatima waongezeka!

Waliopo viongozi, ya watu yarudi nyuma,
Ubinafsi wanaenzi, kwa vitendo na kalima,
Wanajiona waju'zi, nasi hatuna hekima,
Taifa pasipo baba, yatima waongezeka!

Washikilia upuuzi, yenye heri kuyazima,
Na tuhuma za uwizi, zakua kama mlima,
Kulindana ndio kazi, kwa 'ushahidi' hakuna,
Taifa pasipo baba, yatima waongezeka!

Wenyeviti waloenzi, wanaikosa karama,
Wakiahini kizazi, kwa kuupenda uchama,
Kwa njaa nayo hifadhi, mabaya hawatasema,
Taifa pasipo baba, yatima waongezeka!

Kaondoka mwenye hadhi, Mwalimu mwenye kusema,
Vichuguu vyenye ganzi, viko chini ya kilima,
Lenye heri kujajizi, lategemea rehema,
Taifa pasipo baba, yatima waongezeka!

Maisha sasa makazi, na malazi kuyapema,
Na wauza maandazi, huwa hawana rahma,
Huna enzi bila wizi, usio nayo alama,
Taifa pasipo baba, yatima waongezeka!

Baba dunia si mkazi, tumebakia yatima,
Kwa yake makubwa mapenzi, kaiongelea hatima,
Kati yetu wajuuzi, tunaziona alama,
Taifa pasipo baba, yatima waongezeka!

Tunamuomba Mwenyezi, kutuepusha nakama,
Kwa kuwapata viongozi, wa kuzilinda dhuluma,
Ila yaje mapinduzi, kuiondosha nakama,
Taifa pasipo baba, yatima waongezeka!

No comments: