Monday, August 20, 2012

Matapishi wayazoa

Nimeshtuka kugundua, matapishi wanazoa,
Kwenye sahani kutia, na kisha kuyapakua,
Kama kipya kilokuwa, kikawa chapakuliwa,
Matapishi wayazoa, wafanza tena chakula.

Kama kipya kilokuwa, kikawa chapakuliwa,
Na watu wakatengewa, kama mlo kujilia,
Masalo kilipotiwa, uoza haukunukia,
Matapishi wayazoa, wafanza tena chakula.

Harufu yake ni mbaya, kila mtu asikia,
Masalo wanayatia, harufu kuiondoa,
Ila kwa wanaojua, siri wanaifukua,
Matapishi wayazoa, wafanza tena chakula.

Hadaa wanatumia, nyuma yetu kupitia,
Wakubwa wanunuliwa, kamatini walokuwa,
Halmashauri yavia,wastani kutokuwa,
Matapishi wayazoa, wafanza tena chakula.

Wajumbe wanunuliwa, mkutano kuingia,
Uoza kuuchagua, kuongoza Tanzania,
Kuhami waliokuwa, na walivyotuibia,
Matapishi wayazoa, wafanza tena chakula.

Kwa wengi wetu kinyaa, kwao wao yawafaa,
Ujinga wautumia, kuwadhihaki raia,
Miaka ilobakia, wataeneza sanaa,
Matapishi wayazoa, wafanza tena chakula.

Wataeneza sanaa, vifavyo kuvifufua,
Ahadi walizotoa, wizi wakautumia,
Urongo kudanganyia, watu wakaaminia,
Matapishi wayazoa, wafanza tena chakula.

Vijijini wanajua, wajinga watapakaa,
Huko wanawaendea, uongo kwenda wambia,
Kuwa sumu inafaa, sasa chai imekua,
Matapishi wayazoa, wafanza tena chakula.

Kuwa sumu inafaa, kama chakula kuliwa,
Ya uoza ulokuwa, kidonda ndugu kinyaa,
Rais kutupatia, kumalza Tanzania,
Matapishi wayazoa, wafanza tena chakula.

No comments: