Monday, August 20, 2012

Kumbe wanaenda choo...


Saa zinaishilia, na maisha yaishia,
Hakuna la kuongeojea, ukichelea wavia,
Kula wanaojilia, hata wakazidishia,
Kumbe wanaenda choo, muda mrefu kukaa!

Kizuri kinacholiwa, kumbe mate kimetiwa,
Makohozi nayo pia, utamu kuongezea,
Pembeni hujichekea, kwa kila aloandaa,
Kumbe wanaenda choo, muda mrefu kukaa!

Ukubwa kujititimua, njiani wanapokuwa,
Na saluti kupuziwa, shenzi wakaziachia,
Hakuna anayejua, nani moyoni kwingia ?
Kumbe wanaenda choo, muda mrefu kukaa!

Mmoja nimesikia, mlinzi ndani katia,
Eti kisa kutumia, choo cha mheshimiwa,
Afrika ina jaa, mengine kama usaha,
Kumbe wanaenda choo, muda mrefu kukaa!

Watu wanajisheua, vyeo wakivikalia,
Kisha wakaparamia, hata wasiyotakiwa,
Na katiba kupindua, wao juu wakakaa,
Kumbe wanaenda choo, muda mrefu kukaa!

Vidogo wanaugua, makubwa watayajua?
Vyoo vya mheshimiwa, masalo vinanukia,
Ila vya wake raia, utataka kukimbia,
Kumbe wanaenda choo, muda mrefu kukaa!

Islamu tungekuwa, usafi tungeujua,
Udhu kutokuujua, janaba nayo twatembea,
Mola wamsujudia, huku kashfa wamejaa,
Kumbe wanaenda choo, muda mrefu kukaa!

Udi waliojitia, shetani kawapatia,
Na mavumba yamejaa, ni ubani wa chokaa,
Hakuna cha kunukia, kunuka ni maridhia,
Kumbe wanaenda choo, muda mrefu kukaa!

Pepo ya kila msifiwa, kwenye dampu huishia,
Takataka na vinyaa, haachi kuvichukua,
Ingelikuwa mbolea, pengine ingewafaa,
Kumbe wanaenda choo, muda mrefu kukaa!

Tanzu ninamalizia, kuntu nilowaambia,
Hitilafu nimejua, chooni inaanzia,
Mafunzo tukishapewa, ukubwani kuingia,
Kumbe wanaenda choo, muda mrefu kukaa!

Uchafu waujua, kwa kuwa choo waingia,
Mbona wanatuachia, jamii kukanyagia,
Kinyaa chawapotea, au wamekusudia ?
Kumbe wanaenda choo, muda mrefu kukaa!

No comments: