Monday, August 20, 2012

Fakiri aweza jenga



DINI hii ya neema, Mola kaisabilia,
Ukitakia nakama, mwenyewe ukaumia,
Hata zichache tuhuma, kichaa ukaugua,
Fakiri aweza jenga, rais akafulia.

Imani hii heshima, kiumbe ukijaliwa,
Inaamrisha mema, na maovu kukataa,
Na walio na hekima, hawaachi kwitikia,
Fakiri aweza jenga, kafiri akabomoa.

Dini hii ya rehema, usafi yazingatia,
Wafwatao waadhama, haki huipigania,
Inakataa dhuluma, na watu kuwaonea,
Fakiri aweza jenga, tajiri akaagua.

Dini hii ya salama, amani imejaliwa,
Ila shetani kakwama, uzushi anauzua,
Ugaidi wanalalama, Islamu tumekua,
Fakiri aweza jenga, japo katu hana kitu.

Historia kitazama, wao wamechokonoa,
Kwingine kwenda kuzama, kwao kusikokuwa,
Mafuta wakishakwama, ugaidi wanazua,
Fakiri aweza jenga, rais akafulia.

Na nyinginezo tuhuma, Islamu wasingizia,
Viongozi maamuma, uongo wakauvaa,
Wakaikosa heshima, na utu wao kuvia,
Fakiri aweza jenga, kafiri akabomoa.

Ewe mwingi wa rehema, mtambulifu Halimaa,
Kwako twaegemea, huruma na yako afua,
Kuiipitisha karama, yao ukayatengua,
Fakiri aweza jenga, tajiri akaagua.

Zimetuchosha dhuluma, haki tunaililia,
Ngao zako twaazima, ya kwao kuwarudia,
Sisi tubaki wazima, na wao wakaugua,
Fakiri aweza jenga, japo katu hana kitu.


No comments: