Monday, August 20, 2012

Hivi sio ugaidi ?





Mjinga ninauliza, fisadi si ugaidi,
Kweli mkinieleza, utapungua mdadi,
Uchawi nikaapuuza, kwenda kuutaradadi,
Fedha zetu za Uswizi, hivi sio ugaigi?

Mali yetu twapoteza, Waswizi wazifaidi,
Nini kinachotujuza, kuwa hawa si gaidi?
Hamuwezi nieleza, vingine nitakaidi,
Fedha zetu za Uswizi, hivi sio ugaigi?

Wanaizaya wazoza, shetani kutaradadi,
Kila kitu wamaliza, wengine kuwa kuwadi,
Kina babu na ajuza, watakuja zifaidi?
Fedha zetu za Uswizi, hivi sio ugaigi?

Maisha yanateleza, kwetu sisi ni magadi,
Wanatuona uoza, kwa nchi kutofaidi,
Ya kwao wakayakuza, kwa mtaji na miradi,
Fedha zetu za Uswizi, hivi sio ugaigi?

Ni Mola wetu muweza, Muntaqimu kaahidi,
Zawadi atawatunza, kikomo bila idadi,
Ya kwao akayabeza, na wana wasifaidi,
Fedha zetu za Uswizi, hivi sio ugaigi?

Zetu wanazipoteza, wakadai za gaidi,
Wakawa wajipooza, na kula pasi idadi,
Muumba atawazoza, wajitungie nakidi,
Fedha zetu za Uswizi, hivi sio ugaigi?

Juhudi wakihimiza, wao wapandda mdadi,
Siku wanazisogeza, kwenda kula yao iddi,
Azizi ndiye muweza, kaida atakaidi,
Fedha zetu za Uswizi, hivi sio ugaigi?

Tungali twawatazama, ja Huudi na Thamudi,
Sku zao za kuzama, ikifikia mihadi,
Hakuna la kulalama, wala amri kutohidi,
Fedha zetu za Uswizi, hivi sio ugaigi?

No comments: