Monday, August 20, 2012

Hivi sasa ndugu pacha

Waka'ngwa Watanznia, kwa yao wenyewe mafuta,
Hupikwa wakapakuliwa, pasipo hata utata,
Wenye nchi wajilia, wakazidi meremeta,
Hivi sasa ndugu pacha, simu na umaskini!

Wawekezaji wavua, pasipo ya kuchakata,
Sio papa na dagaa, kwenye nyavu utakuta,
Kila siku wavulia, kufulia si wakata,
Hivi sasa ndugu pacha, simu na umaskini!

Dracula wamekuwa, kwa meno wanatung'ata,
Damu wakajinyonyea, na uhai kuupata,
Nyuma tunaobakia, hugeuka mazezeta,
Hivi sasa ndugu pacha, simu na umaskini!

Mashirika twasikia, chama yameshakipata,
Kwetu kinapodonoa, wenye chama wanavuta,
Umelaaniwa ubia, na wanaoupakata,
Hivi sasa ndugu pacha, simu na umaskini!

Siasa wazichagua, na kisha wakazipeta,
Ungo wakatulia, wanasiasa kutota,
Mfukoni wakitiwa, hawawezi kuwasuta,
Hivi sasa ndugu pacha, simu na umaskini!

Nani wa kulibetua, hilo tumeshalipata,
Ni letu la kutundikiwa, budi kuzidi kusota,
Hadi Afu kuamua, nusurra tukaipata,
Hivi sasa ndugu pacha, simu na umaskini!

No comments: