Monday, August 20, 2012

Wajinga wakijanjuka

Ninasema la hakika, mwisho njiani wafika,
Taa inayomulika, hatimaye kuzimika,
Nuru ikatoweka, gizani kuhamanika,
Wajinga wakijanjuka, mjanja hupapatika !

Wajinga waerevuka, na haki yao kutaka,
Sauti inazunguka, na kilio kusikika,
Waliolala waamka, na chao wanakitaka,
Wajinga wakijanjuka, mjanja hupapatika !

Ushindani waumuka, kuupinga ni dhihaka,
Kwa dola kushughulika, raia wakapigika,
Ni ujinga mwautaka, mambo yataharibika,
Wajinga wakijanjuka, mjanja hupapatika !

Demokrasia injika, na chungu kukorogeka,
Nusu nusu ni dhihaka,chakula hakitapikika,
Mzongao mtapwika, na wengine kutapika,
Wajinga wakijanjuka, mjanja hupapatika !

Wajinga wakijanjuka, hadaa huhadaika,
Waliokuwa mateka, kwa bei kununulika,
Ikawa ni kuzuzuka, na kifafa kuanguka,
Wajinga wakijanjuka, mjanja hupapatika !

Umma uliotukuka, unataka madaraka,
Na waporao mamlaka, waziwazi kumulikwa,
Wananchi wana hakika, wao ndio Tanganyika,
Wajinga wakijanjuka, mjanja hupapatika !

Mabaya yaepushika, sauti zikisikika,
Imani zilizowateka, mamluki kuwaweka,
Pembeni zikaondoka, taifa likatukuka,
Wajinga wakijanjuka, mjanja hupapatika !

Ya kundi mkiyashika, umoja utavunjika,
Baragumu lasiikika, na bubu wanatamka,
Haki yao si dhihaka, misuli itatumika,
Wajinga wakijanjuka, mjanja hupapatika !

Uongozi wa dhihaka, haunalo la hakika,
Hubeza ya kuanguka, na kuacha ya kuruka,
Ila Mola akitaka, kila kitu hutoweka,
Wajinga wakijanjuka, mjanja hupapatika !

No comments: