Monday, August 20, 2012

Serikali ya kisasi




Funda saikolojia, kichwani ipae kaa,
Ubaya wazaa ubaya, mnapaswa kutambua,
Ukiwa unayemtia, ukiwa atakutia,
Serikali ya kisasi, ni mama yake maasi.

Kisasi mwana balaa, kwa haramu kazaliwa,
Haki huwa hakataa, sheria wkatukua,
Hasara wakaizaa, mapacha inayozaa,
Serikali ya kisasi, ni mama yake maasi.

Umma mkiuchezea, nao utawachezea,
Wa kuzaa wanazaa, na wao wa kuzaliwa,
Mama asiyemjua, mama humshambulia?
Serikali ya kisasi, ni mama yake maasi.

Aibu ikipungua, uovu hujifungua,
Ni mimba isiyotoa, jema lililojaliwa,
Viroboto huangua, kila kona kuenea,
Serikali ya kisasi, ni mama yake maasi.

Watu ukishawagawa, na hawa kupendelea,
Usawa ukapwelea, kwa wengine ni udhia,
Huja wakajichokea, ahera kuichagua,
Serikali ya kisasi, ni mama yake maasi.

Haki anayeijua, haachi kuipigania,
Dhuluma ukiitia, wazidi kuwacharua,
Haki wakaililia, kwa udhi na uvumba kuwa,
Serikali ya kisasi, ni mama yake maasi.

Jino na kucha kutiwa, maamuzi kuamua,
Pepo wakashuhudia, na msaada kuutoa,
Bendera zikaamua, pande moja kupepea,
Serikali ya kisasi, ni mama yake maasi.

Hekima hutonunua, wala bure ukapwa,
Walo nao kufichua, kazi kubwa sana huwa,
Huzungukwa na nazaa, na rahisi kujilia,
Serikali ya kisasi, ni mama yake maasi.

Jambo hawatakwambia, lakuweza kukufaa,
Sifa watakusifia, na vilemba kukutia,
Ukija kumang'anyua, kokwa jino hulitoa,
Serikali ya kisasi, ni mama yake maasi.

Hali yataka kiasi, kwa pamba si kwa mikasi,
Kamlole muasisi, kwishi pasi wasiwasi,
Ila kwenye kinamasi, huwa maji ya mkosi,
Serikali ya kisasi, ni mama yake maasi.

No comments: