Monday, August 20, 2012

Sheria za kijahili



Sheria za kununua, majaji waliokuwa,
Upande kuegemea, kwingine kutosikia,
Udhalimu unakuwa, kuzifata si sheria,
Sheria za kijahili, kuzikataa sheria.

Wao wakikutumia, ubaya kutufanyia,
Kasumba kuiondoa, juu unahujumiwa,
Kiumbe unapoua, ni wewe uliyeua,
Sheria za kijahili, kuzikataa sheria.

Ukinifanza kulemaa, chanzo nakutambua,
Watu kuwalingania, hofu hii wakatia,
Chombo ni kisafi huwa, damu inajifutia,
Sheria za kijahili, kuzikataa sheria.

Dhambi inajifutia, kwa senti uanzopewa,
Ujinga ukitumia, motoni unajitia,
Nani wa kukuoa, hata wazazi hufulia,
Sheria za kijahili, kuzikataa sheria.

Uongo ukiutia, dhambi unaichukua,
Hata kama wasemea, chama kilichokuwa,
Au serikali kua, sauti ya kutumia,
Sheria za kijahili, kuzikataa sheria

Uwizi ukituibia, hazina vilivyokuwa,
Benkini ukazitoa, wachache kwenda tumia,
Dhambi unaichukua, wala si chama tambua,
Sheria za kijahili, kuzikataa sheria.

Uoza ukisifiwa, na wewe unalaniwa,
Haki ukiisiginia, nyayo zenda kuungua,
Kwa mawe ya mkaa, tayari umewekewa,
Sheria za kijahili, kuzikataa sheria.

Wakubwa wakiamua, uliza na kulijua,
Haki lisilokuwa, kiumbe ni kulikataa,
Mzazi tumeambiwa, si kwa yote kumsikia,
Sheria za kijahili, kuzikataa sheria.

Mzazi tumeambiwa, si kwa yote kumsikia,
Dhambi akituambia, ni budi kulikataa,
Mwenyewe kumuachia, njia zake akajua,
Sheria za kijahili, kuzikataa sheria.

Uslama nausia, salama mtabakia,
Dini wasioijua, inafaa kurejea,
Kubaya mwaelekea, tiketi bure mwapewa,
Sheria za kijahili, kuzikataa sheria.

Mazuri nawatakia, viumbe mojaliwa,
Wakakamavu mkawa, ila njia mwapotea,
Dhuluma manielea, dafrari kuchafua,
Sheria za kijahili, kuzikataa sheria.

Kwa haki mkirejea, mavuno mtaachiwa,
Bora yaliyojaliwa, mikosi isiyokuwa,
Na wana mnaozawa, wasiwe wa kulaaniwa,
Sheria za kijahili, kuzikataa sheria.

No comments: