Monday, August 20, 2012

Mwenge tunaukimbiza, wanariadha hatuna!


AJABU ya Tanzania, kwa mwenge kuukimbiza,
Tope wakaliogea, hakuna wanariadha,
Vipaumbele vavia, masazo kazi kusaza,
Mwenge tunaukimbiza, wanariadha hatuna!

Tanzania yafulia, yabakia kusuza,
Sera zachakachuliwa, hakuna la kuongeza,
Yanazidi kupungua, sifuri tutaikuza,
Mwenge tunaukimbiza, wanariadha hatuna!

Amana wanaopewa, matumbo wanayatunza,
Wenyewe kutangulia, wakafata wanawenza,
Ndivyo inavyotokea, vingine huwezi waza,
Mwenge tunaukimbiza, wanariadha hatuna!

Vijana kuwanyanyua, budi wao kuwatunza,
Mbio watazikimbia, na metali kutunzwa,
Wenyewe tukijilia, tutabakia kuoza,
Mwenge tunaukimbiza, wanariadha hatuna!

Viongozi waogea, wazuri tuliowaza,
Na kinachoambuliwa, chabakia kuongeza,
Njaa yawashambulia, ni nani wa kuwatunza ?
Mwenge tunaukimbiza, wanariadha hatuna!

Mashule yahujumiwa, kwa michezo kuikwaza,
Wawekezaji wavia, vipaji kutovikuza,
Mapambo tumeazimia, nchi yetu kuitunza,
Mwenge tunaukimbiza, wanariadha hatuna!

Kidogo kikibakia, kazi yetu kupoteza,
Twafanza tusokijua, na dira kutoangaza,
Hatujui pa kwendea, vipi tutajiagiza?
Mwenge tunaukimbiza, wanariadha hatuna!

Mashauzi yazidia, na vipozi kutuponza,
Shere tunazochewea, zote twazifurahia,
Hakika mwenye kulemaa, hajui kinachomponza,
Mwenge tunaukimbiza, wanariadha hatuna!

Heshima imepotea, kumbukumbu tunatunza,
Udikteta kuvimbiwa, yote kutaka kufanza,
Mwisho wake waogea, sabuni zilizopooza,
Mwenge tunaukimbiza, wanariadha hatuna!

Twazoea kutumia, sio watu wa kutunza,
Wala kufikiria, yale yanayoingiza,
Kicheko kimebakia, nchi ikaokoteza,
Mwenge tunaukimbiza, wanariadha hatuna!

Mwenge ninadhania, riadha waweza kuza,
Siasa ikitolewa, na manujfaa kuingiza,
Mwenge michezo kwashiwa, kazi ikawa kwendeleza,
Mwenge tunaukimbiza, wanariadha hatuna!


No comments: