Monday, August 20, 2012

Shikilieni huko juu





Ndipo walipoamua, chini kwao kubomoa,
Na juu wakaambiwa, waanze kushikilia,
Watabaki waelea, au waning'inia,
Shikilieni huko juu, wao chini wabomoa!

Dhairi iliyokuwa, hawawezi kununua,
Nyumba nzima kuitwaa, hali bei imepaa,
Kama wakiwachia, na nyumba hawatakuwa,
Shikilieni huko juu, wao chini wabomoa!

Na nchi tarajiwa, juu wakinging'inia,
Chini waweza amua, vyao chini kuvitwaa,
Au kujinyamazia, wabaki kuangalia,
Shikilieni huko juu, wao chini wabomoa!

Jazba ikitumia, wote huwa wafulia,
Nchi ikahujumiwa, na mizizi kung'olewa,
Ya amani ilokuwa, amani, umoja pia,
Shikilieni huko juu, wao chini wabomoa!

Ghorofani wamekaa, chini wawaangalia,
Msiba umetokea, pembeni wanajitia,
Na watu wanapolia, vijisenti wanatoa,
Shikilieni huko juu, wao chini wabomoa!

Msingi wajichimbua, na haki yahakikiwa,
Hesabu ikitolewa, mtazilipa rupia,
Ushahidi wafichua, chini sana kunaliwa,
Shikilieni huko juu, wao chini wabomoa!

Kaeni mlivyokaa, hatima itawajia,
Badili mkibetua, ajali itatokea,
Na mzuka huzuzua, ukweli mnatambua,
Shikilieni huko juu, wao chini wabomoa!

Ya Adilu wasikia, Ya miskin tunalia,
SMS twakutumia, haki ukatutendea,
Subira yatuishia, twataka kusaidiwa,
Shikilieni huko juu, wao chini wabomoa!


No comments: