Monday, August 20, 2012

Wizara hii kiraka





Nafasi hii mashaka, tena mkubwa wahaka,
Kitu kisichobebeka, ibidi kulazimika,
Kwa nguvu kuchukulika, ma watu kuathirika,
Wizara hii kiraka, wabebwaji wabebeka.

Umbeya inaushika, na tuhuma za kuzuka,
Vyomo inavyoshika, dhuluma inafanzika,
Boriti imewatoka, machoni inamulika,
Wizara hii kiraka, wabebwaji wabebeka.

Hawaoni kwa hakika, boriti ilipokalika,
Ila tukitazamika, ya kwetu waimulika,
Wakayazusha mahoka, na riziki kufungika,
Wizara hii kiraka, wabebwaji wabebeka.

Tunamuomba rabuka, ya kwao kuangazika,
Hata wakishughulika, matumbo yakatumbuka,
Na uzushi kuwazika, mihadi ikijafika,
Wizara hii kiraka, wabebwaji wabebeka.

Macho tunayeleka, mbinguni yapepesuka,
Kumuomba mstahika, ya kwetu kutoponzeka,
Na yao yakadhurika, nyumbani na walikoshika,
Wizara hii kiraka, wabebwaji wabebeka.

Walii nayatamka, makubwa yatawafika,
Tawba wasipotaka, nao wakarehemeka,
Wajue walikotoka, na tunakokwenda si hakika,
Wizara hii kiraka, wabebwaji wabebeka.

Ila wakierevuka, iwe kwao ni mashaka,
Waishi kwenye wahaka, na mipango kufumuka,
Waja wakijanjaruka, dua zitakubalika,
Wizara hii kiraka, wabebwaji wabebeka.

Tumevichoka viraka, matakoni kufurika,
Hakuna la kuongezeka, ila ni kupaparika,
Na wakubwa kuwasuka, nywele wasiosukika,
Wizara hii kiraka, wabebwaji wabebeka.

Yangu yanakamilika, fursa nimetosheka,
Wasia nimeshika, kumpa anayetaka,
Na wote wasiotaka, naziondoa baraka,
Wizara hii kiraka, wabebwaji wabebeka.



No comments: