Monday, August 20, 2012

Akaunti za Uswizi



Sio wasiolijua, hilo wameazimia,
Hazina kuchukuliwa, na benki kuu pia,
Kama mbegu zilokuwa, nje kwenda kupandiwa,
Akaunti za Uswizi, chama kukisaidia!

Uchaguzi kiingia, ziende kuchukuliwa,
Na faida kubakia, mwenye jina kujilia,
Kama mnalikaataa, tuone mtu kushtakiwa,
Akaunti za Uswizi, chama kukisaidia!

Chama mnakijua, cha njaa kilojaliwa,
Kinajua kutumia, kutafuta chafulia,
Wabakia kuogea, na taka kuzifagia,
Akaunti za Uswizi, chama kukisaidia!

Makada wanachagua, vya watu kuvichukua,
Nchi wakaitumbua, ila chama kukifaa,
Ila wengi wahadaa, kingi wakakichukua,
Akaunti za Uswizi, chama kukisaidia!

Safu ukiangalia, madini zinatokea,
Hata nayo gesi pia, na petroli zajaa,
Na wanyama kuua, na nje kujiuzia,
Akaunti za Uswizi, chama kukisaidia!

Benki kuu watumia, ni ya chama imekuwa,
Gavana wamtumia, hawezi akakataa,
Ndio maana apewa, vinono akajilia,
Akaunti za Uswizi, chama kukisaidia!

Hazina wazichukua, hata na wizara pia,
Ni chama chasaidiwa, ili kutoenguliwa,
Kumbe watu wajilia, chenyewe kikafulia,
Akaunti za Uswizi, chama kukisaidia!

Mbali sana waanzia, toka makapa kwingia,
Kabla yalijifia, mwalimu kuwaumbua,
Yeye alipojifia, baraka kwao ikawa,
Akaunti za Uswizi, chama kukisaidia!

Awamu wanaizaya, ndiyo hii inapaa,
Benki kuu ilizoa, na hazina nako pia,
Mfukoni wakatia, rais kawakubalia,
Akaunti za Uswizi, chama kukisaidia!

Nao tunawatambua, Arusha wanatokea,
Na Tabora nako pia,chungu walituvunjia,
Kitu kutokubakia, ufakiri kuenea,
Akaunti za Uswizi, chama kukisaidia!

Ndio wanaokusudiwa, urais kuachiwa,
Wa fedha kuzawadia, burushi aliyekuwa,
Ambao wanazichimbua, fedha za Watanzania,
Akaunti za Uswizi, chama kukisaidia!

Madini wamevamia, trilioni wachukua,
Simu wamezikamia, bilioni zawafaa,
Na mafuta nayo pia, hisa wanazipakua,
Akaunti za Uswizi, chama kukisaidia!

Umeme walihadaa, kampuni kuzizua,
Madeni zikatutia, kulipwa siri ikawa,
Hilo linaendelea, huku sisi twaumia,
Akaunti za Uswizi, chama kukisaidia!

Wengine kuruhusiwa, Uswizi kuzichimbia,
Taifa kame likawa, hakuna cha kutumia,
Watu wafa watembea, kwa kiu kali na njaa,
Akaunti za Uswizi, chama kukisaidia!



No comments: