Monday, August 20, 2012

Ufunguo wa bustani



Bustani imefungwa, watu taka wakalia,
Hakuna kilichopangwa, kila mtu atupia,
Mhonga naye mhongwa, pacha sasa wamekuwa,
Ufunguo wa bustani, nimeuweka mfukoni.

Makamasi yanapngwa, na uoza waingia,
Harufu inacharangwa, haramu iliyokuwa,
Wamati[wa ma vichanga, wabakwaji wakizaa,
Ufunguo wa bustani, nimeuweka mfukoni.

Hawalioni ni nongwa, viumbe wametulia,
Ndarahima zawazonga, utuf wakaufulia,
Kuogea wanapangwa, ibilisi kumwogea,
Ufunguo wa bustani, nimeuweka mfukoni.

Masanamu wanachongwa, karne iliyoingia,
Viumbe kutabananga, na sujuda kuzitia,
Wamcha mwenye kuhonga, riziki kumuachia,
Ufunguo wa bustani, nimeuweka mfukoni.

Uongo wanautunga, na vyombo kuviutmia,
Nusura visivyokingwa, ila maovu kulea,
Nafasi zao zazugwa, waja waliopotea,
Ufunguo wa bustani, nimeuweka mfukoni.

Wangojea kujagangwa, ukuu wakapatiwa,
Mikoa wasipopangwa, wilaya huwatumia,
Demokrasia mkunga, haramu yaiandaa,
Ufunguo wa bustani, nimeuweka mfukoni.

Zamani nilishatengwa, na wekundu kuwekewa,
Sikukubali kuzugwa, wakubwa kunitumia,
Waniaga nawaaga, mbalimbali twatembea,
Ufunguo wa bustani, nimeuweka mfukoni.

Mnyonge kama mfungwa, ridhaa hawezi toa,
Kaziye yeye kuchungwa, na bakora kugaIwa,
Na nchi isiyozinga, watu wake huchakaa,
Ufunguo wa bustani, nimeuweka mfukoni.

Huchakaa wakakongwa, na migongo kuugua,
Huku wanakaarangwa, kwa mafuta ya kutoa,
Nafsini wakaengwa, ubaya na umaluni,
Ufunguo wa bustani, nimeuweka mfukoni.

Nafsini wakaengwa, ubaya na umaluni,
Wakakuta wanatengewa, na haki na masikini,
Hapa wameshafinyangwa, kubadili sio nia,
Ufunguo wa bustani, nimeuweka mfukoni.

Mlango haukufungwa, wa saba naupitia,
Yaishia yamnyengwa, kauli sio hatia,
Kwa udugu wanazongwa, mambo yao wafulia,
Ufunguo wa bustani, nimeuweka mfukoni.



No comments: