Monday, August 20, 2012

Kuna meli inazama





Anga nikizitazama, kuna meli inazama,
Upepo unaovuma, chaja kidogo kiyama,
Baharini watakwama, na maziwani kuzama,
Upepo huu wavuma, kuna meli inazama.

Nchi haina uzima, mitumba ndiyo salama,
Bunge lenye taadhima, kwalo hilo wafurama,
Wamenunua lawama,tena ni watu wazima,
Upepo huu wavuma, kuna meli inazama.

Upepo unaroroma, na bahari kungurama,
Na maziwa yazizima, hakuna tena salama,
Na mizuka yaungama, kuvuna kwao rehema,
Upepo huu wavuma, kuna meli inazama.

Njaa yao yawatuma, yasopemwa kuyapema,
Salama inayoyoma, ikabakia zahama,
Na kwao zote tuhuma, zaenda kwa wasoungama,
Upepo huu wavuma, kuna meli inazama.

No comments: