Monday, August 20, 2012

Matajiri Tanzania


Fedha wameitamia, vifarana kuangua,
Wanasiasa wapewa, kesho kutoangalia,
Na vingine wagaiwa, upofu wakawatia,
Matajiri Tanzania, wangojea kutawala.

Benki waliokwapua, na fisadi kuzipewa,
Madeni walioyatwaa, kwa ujanja na hadaa,
Na miradi kuizua, fedha zinakochanua,
Matajiri Tanzania, wangojea kutawala.

Upofu wanawatia, wanaowashtakia,
Na wengine wanaua, kwa yao kukataliwa,
Shetani ajivunia, nchi kuja kuiua,
Matajiri Tanzania, wangojea kutawala.

Matumbo wajishonea, mawili mawili wavaa,
Nafasi ikitokea, lingine huongezewa,
Jetha kawatunukia, hulka yake kutwaa,
Matajiri Tanzania, wangojea kutawala.

Viongozi wanunua, mfukoni wakati,
Na kushoto na kulia, paredi wanatembea,
Ubepari waingia, hata nguo tutavua,
Matajiri Tanzania, wangojea kutawala.

Na wakubwa wenye njaa, uziwi wameingia,
Zama walizozijua, leo wanafiikiria,
Mradi wajipatia, posho wanayopewa,
Matajiri Tanzania, wangojea kutawala.

Hakuna wa kulilia, nchi yake Tanzania,
Kila mmoja kawania, ya kwake kupigania,
Mwalimu kutondokea, balaa zinazaliwa,
Matajiri Tanzania, wangojea kutawala.

Hakuna alobakia, nchi kuigombania,
Kila mmoja awazia, ya kwake yakamfaa,
Na nchi kutochanua, mradi ajipatia,
Matajiri Tanzania, wangojea kutawala.

Na Mola kawaachia, madhambi kujichumia,
Hadi milima ikawa, na toba kutoijua,
Hatimaye kuwavaa, kuwapa yao hidaya,
Matajiri Tanzania, wangojea kutawala.

Ya ovyo wafatilia, ya utu kutoyajua,
Masikini wanalia, michezo washangilia,
Ushindi usiokuwa, wala neema kupewa,
Matajiri Tanzania, wangojea kutawala.

Nchi wanajigawia, na keki ya Tanzania,
Wazawa pipi kupewa, shukrani wakatoa,
Yao yazidi lemea, washindwa kuyachukua,
Matajiri Tanzania, wangojea kutawala.

Siku ninaingojea, machozi kuyaachia,
Taulo ninaandaa, machozi kujifutia,
Tena la kuogeea, kubwa sana lililokuwa,
Matajiri Tanzania, wangojea kutawala.


No comments: