Monday, August 20, 2012

Kaitoeni boriti





Boriti kaitoeni, iliyo mwenu machoni,
Hili mkilibaini, kweli hamtozaini,
Itaisha yaniyani, na visa vya mumiani,
Kaitoeni boriti, mje mbongele njiti.

Ya kwenu kayaoneni, kama yana walakini,
Kisha mje ugenini, kusiko kwenu nyumbani,
Muifanze tathmini, haki inayodhamini,
Kaitoeni boriti, mje mbongele njiti.

Na wa kweli waumini, hupenda nyingine dini,
Hasa wakiwa wahidani, mmoja wamuamini,
Lengo kuu la imani, sote kwingia peponi,
Kaitoeni boriti, mje mbongele njiti.

Kiumbe anayehini, hil tusimuamini,
Hakika ni yake dini, mwenyewe kaleta ndani,
Halifai duniani, mpenziwe ni shetani,
Kaitoeni boriti, mje mbongele njiti.

Kama sivyo majinuni, wameoza akilini,
Wafanyao ni uhuni, shetani awazaini,
Uone wao undani, hukuta hawajiamini,
Kaitoeni boriti, mje mbongele njiti.

Wana mengi maovuni, na mengine mafichoni,
Ndoa hawakuahini, wanazaa duniani,
Usafi kimtihani, waishia sifurini,
Kaitoeni boriti, mje mbongele njiti.

No comments: