Monday, August 20, 2012

Mkichagua viazi





Mkiachagua viazi, hamuwezi kula ndizi,
Uchaguzi una kazi, tena makubwa maamuzi,
Si kitumbua na andazi, mdoni ukakitia,
Mkichagua viazi, hakika mwapata viazi.

Mkipokea viazi, chipsi kupata kazi,
Hii ni nchi ya wazi, si uzuzi na uvumbuzi,
Maisha yake uchizi, taslima na hirizi,
Mkichagua viazi, hakika mwapata viazi.

Kimetokota kizazi, cha uongo na ajizi,
Kimefulia ujuzi, wala sio chapakazi,
Yawaathiri malezi, hawana maandalizi,
Mkichagua viazi, hakika mwapata viazi.

Ni nchi yenye upuuzi, na kuukosa uwazi,
Akili zimebarizi, na bongo za uduwazi,
Kutamba kwa udokozi, na wengine mang'amuzi,
Mkichagua viazi, hakika mwapata viazi.

Sio mabli na ushenzi, na ujirani na nzi,
Vichwa vyetu kama nazi, kuunga tui la mchuzi,
Ndio mwisho maamuzi, kwingine ni mauguzi,
Mkichagua viazi, hakika mwapata viazi.

Yatakiwa mapinduzi, kupisha kipya kizazi,
Mapya kitakachoenzi, na kufanza maenezi,
Wakawa watangulizi, si kudorora kiizi,
Mkichagua viazi, hakika mwapata viazi.

Yaishe ya ulanguzi, na thamani bila kazi,
Tukageuka wajenzi, nchi ikapanda ngazi,
Tuukatae ushenzi, mbu pia na mainzi,
Mkichagua viazi, hakika mwapata viazi.

No comments: