Monday, August 20, 2012

Kawafungueni macho


Wakaanga vijijini, kwa mafuta yao wenyewe,
Hutiwa kikaangoni, kwa vikanga na vikoe,
Na fulana za kijani, waume ziwanunue,
Macho kawafungueni, wamelala vijijini!

Wengi wangali gizani, tongotongo wazitoe,
Wahofia upinzani kutofaa wadhanaie,
Kumbe wana mumiani, ndani wamuaminiye,
Macho kawafungueni, wamelala vijijini!

Vijijini mashakani, kwenye hesabu watoe,
Na sensa kwao utani, ni nani awanyanyue,
Wawatambua mjini, hisani wazitukue,
Macho kawafungueni, wamelala vijijini!

Maji hamna kijijini, ardhi budi ukamue,
Umeme u mipangoni,Bahati wautumie,
Wanauona wayani, juu yao upitie,
Macho kawafungueni, wamelala vijijini!

Toka mwaka wa sitini, pale pale wabakie,
Ubaguzi naamini, lazima uondolewe,
Afrika ya kusini, ndo ule waukatae,
Macho kawafungueni, wamelala vijijini!

Vijijini mikoani, ndio sana walowee,
Hawana lenye thamani, mzazi hana wanawe,
Wakimbilia mjini, wakabakia wazee,
Macho kawafungueni, wamelala vijijini!

Wamelala vijijini, usingizi muwatoe,
Muwajaze akilini, mfumo wauelewe,
Waingie kwa makini, vyamani wavitumie,
Macho kawafungueni, wamelala vijijini!

Wavitumie makini, yao yafanikiwe,
Waiongeze thamani, watu bora wachague,
Kuukuza upinzani, huenda kuwasaidie,
Macho kawafungueni, wamelala vijijini!

Jambo hili ni yakini, kwingine wakatembee,
Wajifunze kwa hisani, kesho yao waijue,
Msiwaache kundini, nje wakatembelee,
Macho kawafungueni, wamelala vijijini!

No comments: