Monday, August 20, 2012

Kila mzuuia wazo



Hawa watu wa uozo, mawazo kwao adui,
Waitafuta mizozo, na tija isiyo hai,
Madhulumu wa matozo, na ziada wanadai,
Kila mzuia wazo, uongozi haumfai!

Uongozi si igizo, latakiwa watu hai,
Wasiofanza gumzo, ila vitendo kutdai,
Na walio na mafunzo, ya filimbi sio nai,
Kila mzuia wazo, uongozi haumfai!

Waliokuwa chelezo, wazo kwao sio rai,
Wanatilia mkazo, yanayotia nishai,
Wayapenda mapumbazo, watu kitu wasidai,
Kila mzuia wazo, uongozi haumfai!

Huo ni wao mchezo, nidhamu hawaijui,
Kila kitu telekezo, heri yao ndugu mwui,
Hufanza kondoo igizo, kumbe hao ndio chui,
Kila mzuia wazo, uongozi haumfai!

Kijibwa mwanavigezo, yaliyomo hayafai,
Na kila mpewa tunzo, amhifadhi adui,
Na kila mwenye mawazo, huonekana hafai,
Kila mzuia wazo, uongozi haumfai!

No comments: