Monday, August 20, 2012

Mwenye uchumi mgeni

Kapewa nchi mgeni, mirija na pia nyuma,
Na kisu cha Kitangeni, kuku akajikatia,
Na wengine hayawani, hayo tukapuuzia,
Mwenye uchumi mgeni, mwananchi afilisiwa.

Mzawa hana thamani, lazima kubaki nyuma,
Kumtanguliza mgeni, wananchi hili lazima,
Mnajua kitu gani, Waafrika mna noma,
Mwenye uchumi mgeni, mwananchi afilisiwa.

Tumuachieni madini, mkuu alishasema,
Tofali kalibaini, pepo yake kaipema,
Jamaa na wake amini, tuhuma zimeshakwama,
Mwenye uchumi mgeni, mwananchi afilisiwa.

Kamwandika Manani, na sisi tunatazama,
Walii hanalo deni, mtaiona sinema,
Kuchuma wasiochuma, wakafulia kazini,
Mwenye uchumi mgeni, mwananchi afilisiwa.

Madaktari yakini, hivi sasa wanahema,
Kuhemea kwarubuni, wamezibwa kwa kalima,
Na pasi hawabaini, kaioneni dhuluma,
Mwenye uchumi mgeni, mwananchi afilisiwa.

Hiki ni kikundi gani, chenye sifa ya unyama,
Na hii ni nchi gani, isiyokwisha lawama,
Na wasema wenye dini, kwetu dalili ya kiyama,
Mwenye uchumi mgeni, mwananchi afilisiwa.

No comments: