Monday, August 20, 2012

Wakubwa wakijiuza


Juu wakinunuliwa, watumwa wa chini huwa,
Ndivyo ilivyo dunia, hainao msamahaha,
Wajiuza kwa kujua, au kwa kutokujua,
Wakubwa wakijiuza, wadogo huwa watumwa.

Wajiuza kwa kujua, au kwa kutokujua,
Yote sawa inakuwa, na utumwa kuingia,
Fedha cheo akapewa, bwana mkubwa akawa,
Wakubwa wakijiuza, wadogo huwa watumwa.

Fedha inaabudiwa, tena sana kutamaniwa,
Watu wakakimbiia, ingawa kupata mkia,
Njiani wakiumia, pasina kujitambua,
Wakubwa wakijiuza, wadogo huwa watumwa.

Shetani ndani kwingia, hata watu kuwagawa,
Ikawa ndugu na jamaa, hakuna wa kuridhia,
KIla aliyejaliwa, hudhani amelaniwa,
Wakubwa wakijiuza, wadogo huwa watumwa.

Hao wakinunuliwa, fedha bwana inakuwa,
Na kila mwenye njaa, rahisi kununuliwa,
Nchi nayo ikizubaa, mnada pia hutiwa,
Wakubwa wakijiuza, wadogo huwa watumwa.

Masikini hubakia, kaziye ni kuiokoa,
Aliyeshiba nazaa, vya kwake kuviachia,
Waachiwa wenye njaa, hujuma kuifumua,
Wakubwa wakijiuza, wadogo huwa watumwa.

Nchi wataiumbua, ikisha kuzainiwa,
Kilio watu kulia, mashaka yakiingia,
Wakuu waliokuwa, kwingine kukimbilia,
Wakubwa wakijiuza, wadogo huwa watumwa.

Marikani wamwachia, hadi ndani kaingia,
Kila nikiangalia, salama sijaijua,
Ndege wanazitumia, kisasi kutugawia,
Wakubwa wakijiuza, wadogo huwa watumwa.

Uranium wachimbua, salama imeshapaa,
Uongo waongopewa, wajinga wahadaiwa,
Kimya kinachotokea, nyuma ya hilo pazia,
Wakubwa wakijiuza, wadogo huwa watumwa.

Waandishi wanunuliwa, uongo kujitungia,
Hidaya wakazipewa, ukweli kuukataa,
Hii ndiyo Tanzania, haya yake majaliwa,
Wakubwa wakijiuza, wadogo huwa watumwa.

Ukombozi watakiwa, safu wasafi wakawa,
Hili ni la kulilia, kuamka na kusinzia,
Mola kutusaidia, mabaya kutwepushia,
Wakubwa wakijiuza, wadogo huwa watumwa.

Vichaka kuviondoa, vilivyojaa balaa,
Wenyewe kujiumbua, mabomu kuwalipua,
Salama tukabakia, kwa Mola tukirejea,
Wakubwa wakijiuza, wadogo huwa watumwa.

No comments: