Monday, August 20, 2012

Shilingi ina medali



Shilingi Olympiki, medali imeileta,
Dhahabu wameafiki, tutunzwe kumeremeta,
Ni kweli siwadhihaki, ikulu wanayateta,
Shilingi ina medali, imeshinda riadha!

Baibai mamluki, watu wanashangilia,
Mapenzi sio riziki, na upendo twafulia,
Tumebakia mashabiki, Uswizi kuzimiliki,
Shilingi ina medali, imeshinda riadha!

Mtanzania mnafiki, aishi kwenye kiota,
Nchini hayaaniki, ila nje yanaota,
Ufalme twaashiki, na ujamaa twasuta,
Shilingi ina medali, imeshinda riadha!

Kulimbikiza mikiki, kila mtu anatweta,
Inawapanda ashiki, nchi wapate pepeta,
Waenziwe kwa milki, ya wenye kiu na njaa,
Shilingi ina medali, imeshinda riadha!

Waisifia kaniki, eti kwayo twatakata,
Wao wanazimiliki, suti zenye kutokota,
Friji zinazodiriki, ndani huwa zakokota,
Shilingi ina medali, imeshinda riadha!

Shilingi amediriki, medali ameileta,
Maisha kuwa hilaki, na utumwa kuuleta,
Wakubwa wayabairiki, na kuyapaka mafuta,
Shilingi ina medali, imeshinda riadha!

Na wala sinayo chuki, mimi siye wa kupata,
Haitakati kaniki, dobi siwezi msuta,
Walo wangu marafiki, wataenzi golgota,
Shilingi ina medali, imeshinda riadha!

Wasema wastahiki, chaguo mola kaleta,
Kweli tunastahiki, taabu kuzikamata,
Tukabakia mabaki, historia kufuta,
Shilingi ina medali, imeshinda riadha!

Waema kaleni keki, kama mkate hamjapata,
Na wala hawadhihaki, hakika si wanaoota,
Hawanao uhakiki, yetu yanavyotokota,
Shilingi ina medali, imeshinda riadha!

Shilingi yangu rafiki, medali unaileta,
Ila kwetu sisi dhiki, maisha yanatokota,
Kwenda usingestahiki, salama tungeipata,
Shilingi ina medali, imeshinda riadha!

No comments: