Monday, August 20, 2012

Huwachukia Kafidi




Viumbe waliokuwa, ukubwa wakijitia,
Ya Mola kuyaumbua, na yao kushindilia,
Katu hatowaridhia, jahanama watapewa,
Huwachukia Kafidi, dini wanaotezea!

Njia pana huachia, watumia wasojua,
Yake kumuharibia, na yao yakatengenea,
Tena yasiyomfaa, na uzushi yalokuwa,
Huwachukia Kafidi, dini wanaoonea!

Huwa anawachezea, paka, panya kumfanzia,
Huru akamuachia, mbali kupiga hatua,
Kisha akamnyakua, mdomoni kumtia,
Huwachukia Kafidi, dini wanaotezea!

Wakwaza kujitambua, ukweli kutojisomea,
Waambiayo kusikia, kisha wakayaabudia,
Ukweli wangeujua, upya wangelizaliwa,
Huwachukia Kafidi, dini wanaoonea!

Waabudu kusinzia, na hadithi kusikia,
Akili wazihofia, hawawezi kutumia,
Dhambi wakajimegea, na mchuzi kujilia,
Huwachukia Kafidi, dini wanaotezea!

Na mchuzi kujilia, uliojaa hadaa,
Wahidi kumchengua, kwa ushirikina ubia,
Wao wakajidhania, kila sawa kimekua,
Huwachukia Kafidi, dini wanaoonea!

Zamani kawaambia, ishara kuzitambua,
Uongozi kutokwaa, akii zinapovia,
Bali zinapotanzua, ukweli zikalilia,
Huwachukia Kafidi, dini wanaotezea!

Waishio kwa kusikia, neno wameshapotea,
Hekaya wazichukua, mashiko yasiyokuwa,
Uongo zilizotiwa, na uhalali kuuawa,
Huwachukia Kafidi, dini wanaoonea!

Kwako nakukimbilia, mtenzi wa kutanzua,
Haki kuniangazia, na wengine kuokoa,
Firdausi kwingia, matunda tukajilia,
Huwachukia Kafidi, dini wanaotezea!

Neno nimeshawaambia, ila hamtoyasikia,
Kubaya mtaemea, hadi roho kutolewa,
Watakaojionea, ukweli watatambua,
Huwachukia Kafidi, dini wanaoonea!

No comments: