Monday, August 20, 2012

Sijui kutengeneza





Mifuko nikishajaza, naipeleka Uswizi,
Siwezi kutengeneza, akili hainitunzi,
Mwepesi kulimbikiza, ila si mtengenezi,
Sijui kutengeneza, budi kuficha Uswizi.

Hulazimu kwenda tunza, palipo watengenezi,
Riba wakaipandikiza, mali nyingi nikahodhi,
Urithi nikautunza, binafsi changu kizazi,
Sijui kutengeneza, budi kuficha Uswizi.

Siwezi kuwaeleza, ya halali au wizi,
Mola kajipendekeza, mimi amenihifadhi,
Ninahofu wanawenza, mnaleta uchokozi,
Sijui kutengeneza, budi kuficha Uswizi.

Nyie nini mngefanza, bahati mngeiridhi,
Mwajitia mngepuuza, fedha nje ziwe wazi,
Au hazina kuoza, kule pasipo na kazi ?
Sijui kutengeneza, budi kuficha Uswizi.

No comments: