Monday, August 20, 2012

Walimu na daktari

Mizani nimetumia, dhuluma naikisia,
Haki wanaolilia, kuzidi kushindiliwa,
Sheria ikalemaa, na dhuluma kuachia,
Walimu na daktari, naoana twawaonea !

Mzigo twawaachia, mlo tunauchukua,
Wao wanapoumia, sisi twazidi tanua,
Na pssho twaongezewa, kujinoma si udhia?
Walimu na daktari, naoana twawaonea !

Vifaa twapuuzia, walimu kufundishia,
Mzigo kuwazidia, hadi jasho kuwatoa,
Jiwe tunang'ang'ania, damu lazima kutoa,
Walimu na daktari, naoana twawaonea !

Keki tukiipakua, nusu nyie mwajilia,
Kidogo kikibakia, bado mnakidokoa,
Kwanini waache kulia, kama si kuwaonea,
Walimu na daktari, naoana twawaonea !

Hali zao zinavia, hadi kuuza vitumbua,
Na michicha na bamia, kazi wasizosomea,
Sisi twawaangalia, twasema ni majaliwa?
Walimu na daktari, naoana twawaonea !

Ulafi umetujaa, juujuu kwenda kaa,
Na tunachowafanyia, madudu tupu yajaa,
Uongozi walemaa, nchi vipi itakuwa?
Walimu na daktari, naoana twawaonea !

Wazungu twawaachia, dhahabu waichukua,
Mengi tusiyoyajua, nayo pia wachimbua,
Yakienda huko Ulaya, mwapewa asilimia?
Walimu na daktari, naoana twawaonea !

Twaona zeu jamaa, ndio bura kuwafaa,
Ngawira kuwagawia, kwingine wakazigawa,
Na safari zazidia, zisizo na manufaa,
Walimu na daktari, naoana twawaonea !

Sasa tunawazuia, na kuwanyima rupia,
Sensa tumewaondoa, ujira hatujatoa,
Vijijini wakimbia, mjini kupumulia,
Walimu na daktari, naoana twawaonea !

No comments: