Monday, August 20, 2012

Asiyetetea haki


Haki asiyetetea, naye ana wake ubaya,
Dhuluma aiachia, wananchi wanaumia,
Hicho anachokipewa, motoni kumchukua,
Haki asiyetetea, dhuluma naye alea!

Huyo naye ni adawa, fukara awaumbua,
Msaada kukataa, awafanzia ubaya,
Thawabu azikimbia, motoni kuungulia,
Haki asiyetetea, dhuluma naye alea!

Kama nasara akiwa, mwana kamkubalia,
Hana kinachopotea, tayari keshautwaa,
Yake anayangojea, zawadi waahidiwa,
Haki asiyetetea, dhuluma naye alea!

Yake anayangojea, zawadi waahidiwa,
Qurani yasimulia, kwa wanayomzulia,
Hili hakufurahia, nao si wa kujitambua,
Haki asiyetetea, dhuluma naye alea!

Hakimu unayepewa, au jaji kuchaguliwa,
Ukiamua sheria, uende kukengeua,
Jua unajiumbua, kwa akhera na dunia,
Haki asiyetetea, dhuluma naye alea!

Madhambi mwajichumia, umma kuutania,
Sisi leo tukilia, milele mwaja kulia,
Huruma nawaonea, viumbe msiojijua,
Haki asiyetetea, dhuluma naye alea!

No comments: