Monday, August 20, 2012

Jimbo hili jimbo langu

Jimbo hili langu jambo, uchuzi pia kijambo,
Waswahili wana mambo, huzungumza matumbo,
Na wengine huwa nyimbo, zikaimbwa na mgambo,
Jimbo hili jimbo langu, upinzani siutaki.

Wazama wenye majimbo, na pepo zaenda kombo,
Wana vikopo vya kimbo, maji kukinga vitambo,
Huenda papo kwa hapo, kuyashibisha matumbo,
Jimbo hili jimbo langu, upinzani siutaki.

Hata wakinuka shombo, wadai kilivyo chombo,
Wakajipasua tembo, kwa kuufata mkumbo,
Hajafumbiwa fumbo, mjinga mwenye kitambo,
Jimbo hili jimbo langu, upinzani siutaki.

Wameyauza machimbo, toka rombo na urambo,
Ardhi bila malambo, watu wapigwa kikumbo,
Ahadi sasa ni wimbo, maneno kuwa mafumbo,
Jimbo hili jimbo langu, upinzani siutaki.

Mchapwa kashika fimbo, mpiga kupigwa kumbo,
Sasa wauza urembo, hata kwa akina gumbo,
Jimbi halijawa jambo, jogoo haimbi wimbo,
Jimbo hili jimbo langu, upinzani siutaki.

Kanyi husema isembo, kwa lugha ni wenye shombo,
Mnasa kala ulimbo, kidaka kubaki nembo,
Hujengi nchi kwa pambo, ni nondo na mitarimbo,
Jimbo hili jimbo langu, upinzani siutaki.

Wasema hajanywa tembo, bali hiyo yake tambo,
Mamaye mama wa kambo, hakumzaa kwa tumbo,
Kalijali lake umbo, ukweli tuseme tumbo,
Jimbo hili jimbo langu, upinzani siutaki.

Namaliza wangu wimbo, kumwimbia mwanakombo,
Maudhui yangu jambo, na halinihusu jimbo,
Nakshi nao urembo, kwangu nahofu ulimbo,
Jimbo hili jimbo langu, upinzani siutaki.

Wanielewa wa Bombo, na kote kwenye machimbo,
Wanihesabu Urambo, hata pia kule Rombo,
Mjinga mfumbie fumbo, mwerevu huzusha tambo,
Jimbo hili jimbo langu, upinzani siutaki.

Husifu kula makombo, ukawa mzuri wimbo,
Kichwani kuweka nembo, mviringo na kitumbo,
Haliwi likawa tembo, walevi wanuka shombo,
Jimbo hili jimbo langu, upinzani siutaki.

No comments: