Monday, August 20, 2012

Vinara wa kupotezea

Wajua kupotezea, kwa kuwa wanahusika,
Rada tumeyang'amua, sasa wanapotezea,
Hakuna mwenye hatia, eti watu tunaambiwa,
Vinara wa kupotezea, washindwe na walaniwa!!

Fisadi weshapotezea, chembani wameingia,
Pesa waliojizolea, yote chama imetwaa,
Mfukoni kuitia, kasri kujijengea,
Vinara wa kupotezea, washindwe na walaniwa!!

Na wengine watembea, kwenye wilaya na mikoa,
uongo kusimulia, hadithi zisizokuwa,
Ujinga tumejaliwa, nasi tunawakubalia,
Vinara wa kupotezea, washindwe na walaniwa!!

Ujinga mkiachia, pabaya mtaingia,
Vipofu wameamua, shimoni kwenda watia,
Nanyi nyuma mwafatia, huku macho mwafungua,
Vinara wa kupotezea, washindwe na walaniwa!!

No comments: