Monday, August 20, 2012

Siwezi kujizuia



VYOTE ninavyotamani, umejaliwa mwandani,
Tabia ninayothamini, na uzuri wa usoni,
Mwili ulio sakini, na ngozi ilo laini,
Siwezi kujizuia, nikaacha kukupenda!

Ni ndoto yangu amini, nikiiota zamani,
Ruia zenye hisani, nikiwaza urulaini,
Kiasi mwangu moyoni, nikajiona jangwani,
Siwezi kujizuia, nikaacha kukupenda!

Msafiri duniani, vijijini na mjini,
Wengi natia machoni, ila hawawi moyoni,
Hadi nilipobaini, utokako mafichoni,
Siwezi kujizuia, nikaacha kukupenda!

Sijalisema kinywani, na kuachia saini,
Cheche zikiwa rohoni, utauliza amini,
Kisha ukaja nyumbani, na wala si mitaani,
Siwezi kujizuia, nikaacha kukupenda!

Nilishachoka moyoni, viumbe sikutamani,
Moto waisha njiani, japo pepo zi makini,
Kisichopo moyoni, sio ashiki mwilini,
Siwezi kujizuia, nikaacha kukupenda!

Nimelipenda jasmini, ua lisilo nuksani,
Harufuye ni makini, inatembeza puani,
Ukitupa kitandani, miski utazaini,
Siwezi kujizuia, nikaacha kukupenda!

Nalitauta yakini, lilipo kwenye bustani,
Mche wake niauni, kuja kupanda nyumbani,
Harufu yake niwini, niwapo mwengu chumbani,
Siwezi kujizuia, nikaacha kukupenda!

Jasmini, asmini, jinalo nalitamani,
Nasibu siiamini, kukupata kilaini,
Ndio niko matesoni, akilini na moyoni,
Siwezi kujizuia, nikaacha kukupenda!


No comments: