Monday, August 20, 2012

Bunge hili bunge gani ?

Bunge hili nchi gani, nani wake waumini,
Ninaishi mashakani, sijui la kina nani,
Naona ni majinuni, imani haimo ndani,
Bunge hili bunge gani, ladharau Ijumaa ?

Dua wanamwomba nani, wanapokuwa bungeni,
Chao ni kitabu gani, cha sala sio ilani,
Nguzo yao nguzo gani, na ibada yao nini ?
Bunge hili bunge gani, ladharau Ijumaa ?

Islamu mwachaguani, kuwakilishwa bungeni,
Watu hao watu gani, walioishiwa imani,
Wanafata ya moyoni, wala si ya imani,
Bunge hili bunge gani, ladharau Ijumaa ?

Anajua majinuni, sheria nazo kanuni,
Wangelikuwa makini, Ijumaa kuamini,
Wakayadai kundini, siku hiyo siyo nuni,
Bunge hili bunge gani, ladharau Ijumaa ?

Mchana uwe wa dini, wafanye kazi jioni,
Kawahadaa shetani, hawapiganii dini,
Wanafiki naamini, ishara wazibaini,
Bunge hili bunge gani, ladharau Ijumaa ?

Nani amesema dini, na siasa haviivani,
Hilo mimi siamini, chama chetu tusaini,
Wakikataa nchini, kiende kichinichini,
Bunge hili bunge gani, ladharau Ijumaa ?

Bunge hili la wahuni, vimini wanatamani,
Tunaapa asilani, sisi kama waumini,
Kuyaiga ya kinuni, tunaenda kitalini,
Bunge hili bunge gani, ladharau Ijumaa ?

Miaka ninabaini, twaenda uchaguzini,
Islamu waumini, chagueni muumini,
Wengine wapige chini, tuongezeke bungeni,
Bunge hili bunge gani, ladharau Ijumaa ?

Ninamuomba Manani, awajaze waumini,
Ushujaa wabaini, kupigania yao dini,
Tumebaki unyongeni, kuanzia Ujerumani,
Bunge hili bunge gani, ladharau Ijumaa ?

Mola tunakuamini, umetujalia dini,
Kuilinda ni auni, kundi hili la amani,
Tutie shime moyoni, tuwaondoe wahuni,
Bunge hili bunge gani, ladharau Ijumaa ?

Tutie nguvu rohoni, yetu yote tubaini,
Tukawalipa wahaini, kwa gharama ya uhaini,
Na kuwalipa hisani, kila mtoa hisani,
Bunge hili bunge gani, ladharau Ijumaa ?

No comments: