Monday, August 20, 2012

Popo wanahangaika

Popo na nduguze hoi, hawajui pa kutua,
Wanalinda maslahi, yasiye yakapotea,
Wauthamini uhai, vitu wanapojaliwa,
Popo wanahangaika, wajiunge pande gani ?

Wazungumzia rai, mojawapo kufikiwa,
Bila ya kupiga nai, na filimbi kusikiwa,
Huku nusu wanadai, unyama unawafaa,
Popo wanahangaika, wajiunge pande gani ?

Nusu hawajitambui, ni ndege wanadhania,
Hawapai asubuhi, ila jioni wapaa,
Mbawa zao maslahi, mbinguni zawachukua,
Popo wanahangaika, wajiunge pande gani ?

Wasema wanajamii, wanyama waumbuliwa,
Kwa kahawa nazo chai, nje wanachukuliwa,
Na sababu hawajui, na wapi wenda kukaa,
Popo wanahangaika, wajiunge pande gani ?

Na sababu hawajui, na wapi wenda kukaa,
Je, watakuwa ni hai, au waenda kuliwa,
Nchi kama haifai, vipi watajirudia?
Popo wanahangaika, wajiunge pande gani ?

Unyama hauwafai, nchi unawakataa,
Heri kuwa ndege mui, maslahi kupatiwa,
Na hii ndiyo rai, wajamaa wasikia,
Popo wanahangaika, wajiunge pande gani ?

Nafusi hawajijui, kazi yao kudandia,
Gauni na sarawilii, haziwezi kutulia,
Waitafuta nikahi, mabibi kuwanunua,
Popo wanahangaika, wajiunge pande gani ?

Chuoni hawachanui, ukubwa waliopewa,
Chini hawaangalii, macho juu wao huwa,
Watamani nani hii, na udugu usiozaa,
Popo wanahangaika, wajiunge kundi gani ?

No comments: