Monday, August 20, 2012

Mkoa hawawakilishi



Hao watu wa kupewa, zawadi wanachukua,
Haki kukutendea, naona haitakuwa,
Humwabudu mteua, kama Mungu kumwofia,
Watu hawawakilishi, viongozi wa mkoa.

Udugu wanatumia, na uchama kuitia,
Bendera ikipepea, wao inawapepea,
Si huru tulokuwa, katika yetu mikoa,
Watu hawawakilishi, viongozi wa mkoa.

Kampenzi zanunua, kapuni zikawatia,
Sababu nchi kuvia, ni wakuu wa mikoa,
Ya watu kutoyajua, chama kukifikiria,
Watu hawawakilishi, viongozi wa mkoa.

Wengine wanatumiwa, watu yao kuibiwa,
Madini yaliyojaa, na haki za kidunia,
Kisha wawashindilia, na risasi kutumia,
Watu hawawakilishi, viongozi wa mkoa.

Viwanja huvichukua, wenyewe kujigawia,
Na mashamba nayo pia, kupona haitakuwa,
Yote wanayamavia, ubepari kuchipua,
Watu hawawakilishi, viongozi wa mkoa.

Ndani wanawatumia, na nje kuwauzia,
Haki kwao sio nia, ila nia kujilia,
Hawatetei raia, mkubwa wamtetea,
Watu hawawakilishi, viongozi wa mkoa.

Watu wawashambulia, upinzani kama wawa,
Kwao demokrasia, ni ufalme kuridhia,
Wameila hadaa, kutapika wakataa,
Watu hawawakilishi, viongozi wa mkoa.

Si wema walokuwa, Mtwara ukiangalia,
Dini zinawatumia, wakijidai watawa,
Mambo wawafanyia, ndugu zaburi yajua,
Watu hawawakilishi, viongozi wa mkoa.

Imani wakihofia, watu watawaonea,
Yao wakayakataa, na uzushi kuwazushia,
Mola haachi chukia, akawaona udhia,
Watu hawawakilishi, viongozi wa mkoa.

Bure tu hujifutua, kwa dola kuitumia,
Dua tukiwaombea, ulemavu wauvaa,
Waumini mwatakiwa, mamb haaya kuyajua,
Watu hawawakilishi, viongozi wa mkoa.

Dini ikijitambua, mbali nao itakaa,
Serikali hufatia, Mungu anatangulia,
Jihadi tunajua, ni amri tumepewa,
Watu hawawakilishi, viongozi wa mkoa.

Kiumbe ukijifia, dini yao kutetea,
Peponi utaingia, mambo mema kuridhiwa,
Mola kumsabilia, ni chaguo lake huwa,
Watu hawawakilishi, viongozi wa mkoa.

Ubwana wanajitia, na utwana kututia,
Tunu inayowafaa, madarakani kung'oa,
Wengine tukachagua, viongozi wetu kuwa,
Watu hawawakilishi, viongozi wa mkoa.

No comments: