Monday, August 20, 2012

Dini mkizibagua





Mamlaka mkipewa, haki budi kutambua,
Kisha kutokuegemea, upande mmoja mkawa,
Taifa litaugua, na msibani kwingia,
Dini mkizibagua, huvuna matunda haya.

Nchi haina ubaya, viumbe ndio wabaya,
Hasa wanaotumiwa, na watu kununuliwa,
Ovyo wakajifanzia, na kinyesi kujitia,
Dini mkizibagua, huvuna matunda haya.

Haki wakainunua, na mengine kuchukua,
Ukubwa wakajitia, na utakatifu pia,
Kumbe uoza wakawa, na nchi kuisumbua,
Dini mkizibagua, huvuna matunda haya.

Shilingi huitumia, heshima kujipatia,
Na vyeo wakavipewa, kisomowasichojua,
Na kazi wasizozijua, kila siku kupangiwa,
Dini mkizibagua, huvuna matunda haya.

Vipofu kazi hupewa, macho za kutarajia,
Na viziwi nao pia, kazi za kusikizia,
Kicheko kuanguliwa, ikitazama dunia,
Dini mkizibagua, huvuna matunda haya.

Mola mwenye kutambua, dini ameziachia,
Madhehebu kujigawa, na yao kujifanzia,
Ukweli yaliokuwa, na waongo nao pia,
Dini mkizibagua, huvuna matunda haya.

Ya kwako ni kujifanyia, wengine kutoingilia,
Vingine inavyokuwa, ubaya mwauchimbua,
Viongozi wa ridhaa, hili watalikataa,
Dini mkizibagua, huvuna matunda haya.

Juu mnapokalia, ya chini kuangalia,
Kwa haki pia usawa, msije kuchakachua,
Na nchi ikaugua, na watu kuja umia,
Dini mkizibagua, huvuna matunda haya.


No comments: