Monday, August 20, 2012

Ombaomba kwenye suti

Wanashangaa umati, ombaomba kujionea,
Ana tai kwenye suti, na viatu vya kupaa,
Aonekana smati, watu wanamkimbia,
Ombaomba kwenye suti, ajabu ya Tanzania!

Akiitoa sauti, wadhani anatania,
Sasa kizungumkuti, kichwa kajiinamia,
Huyu ndiye mahuluti, ubepari-ujamaa,
Ombaomba kwenye suti, ajabu ya Tanzania!

Mavazi kayadhibiti, watu wajua kajaa,
Akisema haileti, watu wadhani kichaa,
Na hakuna katikati, ukweli wa kumwambia,
Ombaomba kwenye suti, ajabu ya Tanzania!

Anapopiga magoti, kusali wanadhania,
Mhubiri madhubuti, wengine washadidia,
Masikini hawateti, wasije kumuumbua,
Ombaomba kwenye suti, ajabu ya Tanzania!

Ana gari la spoti, na bembeya kubembea,
Uswizi kaficha noti, wenye njaa kawaibia,
Na bungeni hawalileti, siri yao wanajua,
Ombaomba kwenye suti, ajabu ya Tanzania!

Kimo chake nusu futi, milingoti atumia,
Ukimuona shurti, kucheka huwa tabia,
Kwenye mvua hatoti, mwamvuli kauchukua,
Ombaomba kwenye suti, ajabu ya Tanzania!

Wanamuita steti, hati asiyepatiwa,
Kuingia kuna geti, mahala anapokaa,
Tukutuku huileti, lazima itazuiwa,
Ombaomba kwenye suti, ajabu ya Tanzania!

Wameshamtuku cheti, ombaomba kumjua,
Wakiangalia kabati, ndarahima zimejaa,
Kuomba hawamsuti, wataka kumtumia,
Ombaomba kwenye suti, ajabu ya Tanzania!

Ah, nchi isiyo bahati, na unafiki kujaa,
Kitanda cha asherati, na nyinginezo balaa,
Halali hauikuti, ni haramu imejaa,
Ombaomba kwenye suti, ajabu ya Tanzania!

Naiangaza tovuti, ukweli ukasambaa,
Dhana hii ni katiti, kimo haijagaiwa,
Na kwangu halitakati, ni chafu lilokuwa,
Ombaomba kwenye suti, ajabu ya Tanzania!

Naamini mkakati, waliomo wafulia,
Na kuingiliwa kati, ushauri wakataa,
Wanailea boriri, kijiti wakiumbua,
Ombaomba kwenye suti, ajabu ya Tanzania!

Nipe shehe Mtengeti, nami ninakuachia,
Tano zaidi sileti, ujumbe unshatulia,
Kumbe Mista Raiti, kufika amechelewa,
Ombaomba kwenye suti, ajabu ya Tanzania!

No comments: