Wednesday, July 18, 2012
Mnyonge ana sauti
WAO ni kama maiti, nani wa kuangalia,
Waliokalia viti, mengine yawasumbua,
Mnyonge hana bahati, kaziye kuhujumiwa,
Mnyonge ana sauti, ushairi kupitia !
Hukisiwa afriti, mengi akitumumiwa,
Hata ndugu humsaliti, jaha kuikimbilia,
Akaishia makuti, na donge la kukandia,
Mnyonge ana sauti, ushairi kupitia !
Ya kwake hawayateti, wala kuzungumzia,
Yakitiwa kwenye hati, msaada watakiwa,
Fukara haumkuti, mifukoni huishia,
Mnyonge ana sauti, ushairi kupitia !
Wala hanayo kamati, yake yakafikiriwa,
Hakuna ya kweli dhati, umaskini kutoa,
Mambo yao hatihati, wenyewe kujipalilia,
Mnyonge ana sauti, ushairi kupitia !
Fukara haumkuti, mifukoni huishia,
Kwa wenye kuvaa suti, na ghorofa za kofia,
Maskini kibushuti, hana anachoambulia,
Mnyonge ana sauti, ushairi kupitia !
Mnyonge hana bahati, kaziye kusahauliwa,
Au kama kibiriti, hutumika kuwashia,
Na mezani hakiletwi, mtu kikishamfaa,
Mnyonge ana sauti, ushairi kupitia !
Ni mtumwa wa vicheti, na vya bure vibarua,
Zoezini humkuti, ila kwenye kuhesabiwa,
Anazo nyingi shuruti, vizuri kutawaliwa,
Mnyonge ana sauti, ushairi kupitia !
Mwanaye hali biskuti, wala kupewa halua,
Daraja la pili si kati, hilo kaishachaguliwa,
Hata akiwa 'smati', ndipo hapo huishia,
Mnyonge ana sauti, ushairi kupitia !
Yananiuma magoti, nashindwa kuendelea,
Ila wasia wa dhati, huu nishawaambia,
Mazuri hatuyakuti, mnyonge tumimuonea,
Mnyonge ana sauti, ushairi kupitia !
Mshairi siwasaliti, nazidi kuwatetea,
Hadi nipate mauti, na wengine kuachia,
Namuomba Muqsiti, daima kuangalia,
Mnyonge ana sauti, ushairi kupitia !
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment