Wednesday, July 18, 2012

FIDIA YETU UHUNI

Ndio ma'na wanaua, fidia zetu dhihaka,

Maisha ya Mtanzania, thamani hatujaweka,

Vishilingi twalipia, mpewa akajicheka,

Fidia zetu dhihaka, ndio ma'na tunaaua !

Watazungumza wanaa, na Mola kumzulia,

Ila wa mtu ukiwa, mkono tunaujua,

Muhyi huwasaidia, wanaojisaidia,

Fidia zetu dhihaka, ndio ma'na tunaaua !

Tajiri watutania, ni wa kufa na kuzika,

Thamani waitambua, milioni kutofika,

Vijisenti watambua, hawawezi pepesuka,

Fidia zetu dhihaka, ndio ma'na tunaaua !

Wakubwa wamewatia, mfukoni kuwaweka,

Yao wanayaelewa, wana njaa za kunuka,

Nani wa kuwatishia, thamani kuongezeka ?

Fidia zetu dhihaka, ndio ma'na tunaaua !

Mahakama wazishika, rahisi zitaamua,

Hawawezi filisika, biashara kwendlea,

Wao hawana mashaka, ni Mungu ameamua !

Fidia zetu dhihaka, ndio ma'na tunaaua !

Hawa ni Waafrika, ndiyo yao kugundua,

Ukija umefyatuka, yaweza kukutokea,

Bila kanuni kuweka, na wageni watalia,

Fidia zetu dhihaka, ndio ma'na tunaaua !

Safari zetu mashaka, na ajali majaliwa,

Tajiri hatoteseka, masikini huumia,

Kisha huzuka vizuka, ya uongo wakalia,

Fidia zetu dhihaka, ndio ma'na tunaaua !

Wanga watadaamka, na machozi kuyatoa,

Kumbe wao ndo mahoka, kisa kilichochangia,

Maiti wakasifika. pengo wametuachia,

Fidia zetu dhihaka, ndio ma'na tunaaua !

Pengo likaelezeka, na wasifu kuutoa,

Hawawezi kuzuzuka, kazi wameizoea,

Ya mnyonge patashika, ndiyo aliyojaliwa,

Fidia zetu dhihaka, ndio ma'na tunaaua !

No comments: