Wednesday, July 18, 2012

Kwenye waongo na wezi








BALAA huzaliana, zikawa kadha wa kadhaa,

Tena zikafuatana, kama kunywesha mvua,

Hutupima Maulana, kuona kama twamjua,

Kwenye waongo na wezi, balaa huzaliana!



Yanawashinda mchana,kutafutia dawa,

Usiku wakachuana, gizani kuulizia,

Ajizi nyumba ya laana, na mkewe ni makiwa,

Kwenye waongo na wezi, balaa huzaliana!



Mitumba wamependana, ya meli watulettea,

Miaka hawajaiona, wala hawataijua,

Kufa kwao kufaana, mifuko huzidi jaa,

Kwenye waongo na wezi, balaa huzaliana!



Mengi sana watanena, tukio likishatukia,

Mipango hutoiona, sembuse zao hatua,

Mambo huwa yalandana, kama zama yatakuwa,

Kwenye waongo na wezi, balaa huzaliana!



Chozi la mamba lanona, uchungu hataujua,

Kina mama nao wana, ndio wanaoumia,

Wakitoweka mabwana, nani kuwaangalia ?

Kwenye waongo na wezi, balaa huzaliana!



Nywele ngumu na kitana, watawala wamekuwa,

Hakika hawatonena, simulizi watatoa,

Na mola washaachana, waabudu ya dunia,

Kwenye waongo na wezi, balaa huzaliana!



Yunusi alishaona, na siri anaijua,

Kwetu hawana maana, wajifanzao wajua,

Ni yanini kubishana, sineme kujionea,

Kwenye waongo na wezi, balaa huzaliana!



Huja yakajaumana, mioyo kuifufua,

Ikaondoka hiyana, na wakweli kujaliwa,

Imani waliyoshona, Muumba kumgeukia,

Kwenye waongo na wezi, balaa huzaliana!



Waache wenye kukana, ya kwao wanayajua,

Leo wana muamana, kesho huwatumbukia,

Nyongo zikawa suna, na faradhi papo pia,

Kwenye waongo na wezi, balaa huzaliana!



Mola wangu Maulana, hifadhi naililia,

Hawa wakwetu mabwana, yangu wameshafulia,

Umebakia utwana, na pekee majaliwa,

Kwenye waongo na wezi, balaa huzaliana!

No comments: