Wednesday, July 18, 2012

Wanautaka ukubwa






WASUMBUKAO kwa njaa, ya ukubwa kuukwaa,

Fumbo nimelifumbua, kuongoza hufulia,

Wakawa wang'ang'ania, watu huku waumia,

Wanautaka ukubwa, kuongoza hawawezi !



Njaa yao kutumbua, vya umma wakajilia,

Wala si kusaidia, na watu kuwanyanyua,

Yao wamedhamia, siye nyie kuwafaa,

Wanautaka ukubwa, kuongoza hawawezi !



Ukubwa wanadhania, ni nafasi kuchukua,

Kichwani wakawa wang'aa, kwa utupu kuuvaa,

Hawana la kuamua, la wananchi kuwafaa,

Wanautaka ukubwa, kuongoza hawawezi !



Ni mzigo wanakuwa, mabegani mwa raia,

Badala kuendelea, huwa tunadidimia,

Lakiini watajisifia, eti twapiga hatua,

Wanautaka ukubwa, kuongoza hawawezi !



Kaitazame Malaysia, au nayo Indonesia,

Udhia utatambua, na dhihaka kuagua,

Kila mwenye kujisifia, kasoro nyingi kajaa,

Wanautaka ukubwa, kuongoza hawawezi !



Vya msingi twaachia, ugaidi tunalia,

Ya kwetu twayaachia, ya wazungu kuchukua,

Ila si yanayofaa, bali wao kuridhia,

Wanautaka ukubwa, kuongoza hawawezi !



Juu wanakobakia, ndiko wanaishilia,

Ya chini hawatajua, uongo watagawiwa,

Ajizi kupakuliwa, wakala na kucheua,

Wanautaka ukubwa, kuongoza hawawezi !



Ujinga unatuua, ya kwetu kutotambua,

Haya yanapotokea, watu tunawaaachia,

Na Mungu kumzulia, ya shetani yalokuwa,

Wanautaka ukubwa, kuongoza hawawezi !



Shetani achekelea, Mola kumsingizia,

Na namba anatutia, wajihini zikang'aa,

Hakika tutakijua, nachelea, nahofia,

Wanautaka ukubwa, kuongoza hawawezi !



Tupe nafuu jalia, uongozi wa kufaa,

Hali kuzia.ngalia, na kupungua nazaa,

Tuvute kukurudia, tukakimbia hadaa,

Wanautaka ukubwa, kuongoza hawawezi !





No comments: